Na Albano Midelo,JamhuriMedia,Mbinga
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan Imetoa zaidi ya shilingi milioni 560 kupitia program ya Uboreshaji Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kujenga sekondari mpya wilayani Mbinga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Amina Seif amesema sekondari hiyo mpya inajengwa katika Kata ya Matarawe ambapo ujenzi wake utahusisha vyumba vinne vya madarasa,ofisi moja ya walimu,jengo la utawala,maabara tatu, maktaba, chumba cha TEHAMA,vyoo,kichomeaa taka na tanki la maji.
Hata hivyo Seif amebainisha kuwa Halmashauri hiyo hivi karibuni imepokea jumla Shilingi Milioni 655,552,827.00 kati ya fedha hizo shilingi 560,552,827 ni kwa ajili ya ujenzi wa sekondari mpya ya kata ya Matarawe na shilingi milioni 95 ni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mwalimu ya familia mbili katika sekondari ya Lusonga.
“Kwa niaba ya wananchi wa Mbinga,namshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuletea fedha za kuboresha miundombinu ya elimu katika Halmashauri yetu hali ambayo itasaidia kuboresha elimu ya awali,msingi na sekondari’’,alisema.
Ameahidi kusimamia matumizi ya fedha hizo na kuhakikisha mradi wa ujenzi wa miundombinu hiyo ya elimu unakamilika kabla ya Oktoba 30,2023.
Serikali kupitia program ya SEQUIP katika wilaya Mbinga imetoa zaidi ya shilingi bilioni 1.8 kujenga shule mpya za sekondari katika kata za Lusonga,Amanimakoro na Matarawe.