Na Mwandishi wetu, JAMHURI MEDIA, Nairobi
Katibu mkuu wa chama cha upinzani cha ODM nchini Kenya ambaye pia ni Seneta wa jiji la Nairobi Edwin Sifuna ameitisha maandamano ya siku tatu kuanzia wiki ijayo, akiapa kuzidisha maandamano dhidi ya serikali hadi matakwa yao yatakapotekelezwa.
Kulingana na Sifuna, maandamano hayo ya siku tatu kila wiki yatafanyika kuanzia Jumatatu hadi Jumatano na yatakamilika tu wakati Rais William Ruto atakapokubali kupitia upya Sheria ya Fedha ya 2023 yenye utata.
“Kuanzia wiki ijayo, siku tatu mfululizo za maandamano, Jumatatu, Jumanne, Jumatano hadi William Ruto atakapoelewa kuwa watu wanateseka na kubatilisha sheria hii jinsi alivyoiweka juu yao,” alisema.
Akizungumza katika kipindi cha runinga ya Citizen mapema leo Alhamisi , alisema kwamba serikali inafaa kusikiliza matakwa ya Wakenya wengi kabla ya kuchukua suala hilo mikononi mwao.
“Ni afadhali wakati huu ambapo watu kama Sifuna, Raila, Osotsi (Seneta wa Vihiga), wanaongoza maandamano haya. Siku Wakenya watakaposhughulikia suala hili wenyewe hakutakuwa na mtu wa kuwaita kwenye meza,” alisema.
Pia aliikemea serikali kwa kutangaza awali kuwa itawakamata viongozi wa Azimio wakidai kwamba hawatarudi nyuma katika vita vya dhidi ya serikali na wako tayari kukamatwa kwa sababu hiyo .
“Hakuna mtu atakayetutishia. Hakuna kitu ambacho hawa watu (Kenya Kwanza) hawajasema. Hakuna wanachoweza kututisha nacho. Ikiwa ni kukamatwa tuko tayari,” alibainisha Sifuna.