Balozi wa Tanzania Nchini Cuba Humphrey Polepole amesema waasisi wa Mataifa ya Afrika walifanya jukumu lao kwa harakati kubwa za kulikomboa Bara la Afrika na kwamba ni wakati wa kizazi cha sasa kuhakikisha wanaleta ukombozi wa kiuchumi barani na njia pekee ya kufanikisha hilo ni kuzungumza lugha moja ya Kiswahili.
Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania Havana kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Havana, Nyumba ya Afrika na Serikali ya Cuba,yamehudhuriwa na mabalozi wa nchi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini Cuba, wawakilishi wa wizara mbalimbali, Taasisi za Umma na Binafsi pamoja na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Havana.
Kiswahili hadi sasa tayari kinatambulika kama miongoni mwa lugha rasmi kwenye Muungano wa Afrika, na kinatumika kama lugha rasmi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na Bunge la Afrika na ni moja ya lugha za Afrika zinazozungumzwa na watu wengi duniani.
Ikumbukwe kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu , sayansi na utamaduni UNESCO Novemba 23, 2021 lilitangaza rasmi tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani.