Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Same
Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni ametoa mwezi mmoja kwa viongozi wa vijiji vitatu vya Tae, Mahande na Heikondi vilivyo kata ya Tae wilayani humo kushirikiana kuteketeza mashamba yote ya mirungi na kuachana na zao hilo haramu.
Ameagiza viongozi wa Halmashauri kusimamia utekelezaji huo na kutumia wataalam wa Idara ya kilimo kufanya utafiti na kuainisha mazao mbadala yanayostawi katika eneo hilo, na kutoa elimu kwa wananchi waweze kunufaika.
Mkuu wa Wilaya Mgeni ameyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara maalum uliokuwa unalenga kuzungumzia kazi ya utekelezaji wa kuteketeza mashamba ya mirungi linaloongozwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za kulevya wakishirikiana na vyombo vingine vya usalama.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)Aretas Lyimo amesema oparesheni hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt.Samia Suluhu Hassani ambapo wamefanikiwa kuteketeza ekari 535 katika vijiji hivyo vitatu ndani ya siku saba.