Na Immaculate Makilika, JamhuriMedia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa ni mfumo wa kisheria unaoziwezesha nchi kushirikiana katika kuzuia vitendo vya rushwa, katika kuwachunguza watuhumiwa wa makosa ya rushwa pamoja na urejeshwaji wa mali zilizotokana na vitendo vya rushwa katika nchi husika, kubadilishana watuhumiwa wa makosa ya rushwa waliotoroka nchi zao na kubadilishana taarifa na ushahidi.
Aidha, Mkataba huo umeweka misingi ya kisheria ya nchi za Afrika kushirikiana katika mafunzo ya kiweledi yanayohusu namna ya kuzuia na kupambana na rushwa na kupeana misaada ya kisheria pamoja na ushirikiano wa kiufundi katika kushughulikia kwa haraka maombi ya vyombo vyetu tulivyovipa jukumu la lazima la kuzuia, kutambua, kuchunguza na kuadhibu washtakiwa wa makosa ya rushwa.
Hayo yamelezwa leo Julai 11, 2023 jijini Arusha na Rais Samia wakati akihutubia katika Kilele cha Maadhimisho ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika.
“Natoa rai kwa wadau wote wa mapambano dhidi ya rushwa kutafakari na kuchambua kwa dhati masuala haya ili kubainisha changamoto au vikwazo vya mapambano haya na kuchukua hatua muafaka, wala rushwa wanapaswa kufahamu kwamba nchi zetu si vichaka vya kuficha fedha zilizotokana na rushwa au kufuga wala rushwa. Tunataka dunia nzima ifahamu kuwa, Afrika sio salama kwa wala rushwa, na hilo lionekane kwa vitendo kupitia hatua tunazozichukua dhidi ya wala rushwa na sio mikutano, makongamano na maneno peke yake”, alisema Rais Samia.
Amefafanua hatua iliyopigwa na Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kusema kuwa, Tanzania imewekeza zaidi katika matumizi ya mifumo ya teknolojia ya habari kwa huduma ambazo si lazima yawepo mawasiliano ya mtu na mtu ili kupunguza tatizo la kuzungumza na kupatana, na kuwa tayari Tanzania inatumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika michakato mbalimbali ikiwemo ya zabuni, usajili wa biashara, namba ya mlipa kodi na maombi ya kuunganishiwa umeme.
“Pamoja na juhudi hizi, bado jitihada zinahitajika kukabiliana na janga la rushwa kwa njia za kiuadilifu na ufanisi zaidi, hivyo imeanzishwa divisheni ya Mahakama Kuu inayosikiliza kesi zinazowahusu washtakiwa wa makosa ya rushwa kubwa. Kwa kuanzia mwaka wa fedha 2019/20 hadi 2021/22, tulifanikiwa kuokoa na kudhibiti matumizi ya fedha yasiyostahili ya zaidi ya shilingi bilioni 139, hiki ni kiasi kikubwa kwa fedha za umma”, amebainisha Rais Samia.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika, Paschal Antonio Joachim amesema kuwa miaka 20 iliyopita, Umoja wa Afrika ulifanya maamuzi muhimu kwa kuidhinisha makubaliano ya kuwa na chombo cha pamoja ambacho kimewekwa kama mfumo wa nchi za Afrika ili kuweza kudhibiti na kupambana na rushwa.
“Tunaendelea kufanya shughuli zetu ili tuweze kuwa na Afrika tunayoitaka sisi, ambayo ina Demokrasia, Utawala Bora, inaheshimu Haki za Binadamu na Utawala wa Sheria. Aidha, ninampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuchukua muda wake na kushiriki katika Maadhimisho haya ya Kupambana na Rushwa Afrika”, amemaliza Joachim.