Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la kujenga Taifa ( JKT ) Julai 10,2023 Jijini Dodoma.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashungwa amesema hayo leo Julai 8,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari na kutumia nafasi hiyo kuwaalika wananchi wote, Viongozi wa Serikali, Taasisi mbalimbali na watumishi kujitokeza kwa wingi kuhudhuria siku ya kilele cha maadhimisho hayo.

Amesema,”Nawakaribisha wananchi wote wajitokeze kuhudhuria siku ya Jumatatu kuanzia saa 12:30 asubuhi katika uwanja wa Jamhuri wa Dodoma, kutakuwa na gwaride la vijana wa JKT,maenesho ya vifaa mbalimbali vya SUMAJKT na burudani za ngoma kutoka vikundi vya JKT na wasanii mbalimbali,”amefafanua na kuongeza;

“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa jitihada anazozifanya na kuhakikisha JKT linaendelea kuwa kitovu cha malezi bora kwa vijana wa kitanzania” amesema Waziri Bashungwa

Waziri huyo pia amesema kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya JKT kimetanguliwa na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na JKT Marathon 2023 iliyofanyika June 25 jijini Dodoma.

“Hii ni marathon ya kwanza kuandaliwa na JKT tangu kuanzishwa kwake na ilifana sana,pia Makamu wa Rais DK. Philip Mpango mnamo julai 1 ,2023 alifanya uzinduzi wa mnara wa kumbukumbu makao makuu ya JKT yaliyopo Chamwino Dodoma na kufungua maonesho ya bidhaa siku hiyo hiyo ambayo yanaendelea mpaka sasa katika viwanja vya Medeli East mkabala na SUMAJKT House,”ameeleza.

Pamoja na hayo Waziri Bashungwa amesema kuwa Katika maadhimisho hayo JKT pia walifanya shughuli za kijamii kama kutembelea hospitali ya Uhuru iliyopo wilaya ya Chamwino pamoja na vituo vya kulelea watoto wenye uhitaji .