Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Chato
SERIKALI imezindua rasmi mashindano ya mpira wa miguu “Chato Samia Cup 2023” kwa lengo kutambua jitihada kubwa za rais Samia Suluhu Hassan,katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye wilaya ya Chato mkoani Geita.
Aidha Chama cha mpira wa miguu wilayani hapa (CDFA) kimetoa baraka zote za mchezo huo ambao utalindima katika viwanja mbalimbali kwa takribani miezi miwili.
Mashindano hayo ni ya kwanza kuasisiwa kwenye wilaya ya Chato,tangu rais Samia kutwaa madaraka kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wa Tanzania,Hayati Dk. John Pombe Magufuli,ambaye alifariki kwa tatizo la moyo kisha mazishi yake kufanyika nyumbani kwao kijiji cha Mlimani rubambangwe wilayani hapa.
Akizindua mashindano hayo kwa niaba ya Naibu waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo,Hamis Mwijuma (Mwana FA), Mkuu wa wilaya ya Bukombe,Said Nkumba,ameitaka jamii kutumia michezo hiyo kuibua vipaji vilivyo lala kwa madai kuwa mchezo wa soka kwa sasa unatoa ajira kubwa na kuinua uchumi wa kaya na familia kwa ujumla.
Mbali na mchezo huo, amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ikiwa ni ishara ya kuenzi kazi kubwa za maendeleo zinazotekelezwa na rais Samia kwenye wilaya hiyo ikiwemo baadhi ya miradi iliyoachwa na mtangulizi wake Hayati Dk. Magufuli.
Akiongea na umma wa wanamichezo waliojitokeza kwenye viwanja vya shule ya msingi Katemwa Muganza,Mkuu wa wilaya ya Chato, Mhandisi Deusdedith Katwale,amesema wameamua kutumia mchezo wa soka kuwaweka watu pamoja ikiwa ni pamoja na kutambua kazi kubwa zinazotekelezwa na rais samia katika kusukuma maendeleo ya wananchi.
Amezitaja baadhi ya sekta zilizopewa fedha nyingi za utekelezaji kwenye wilaya hiyo kuwa ni miundo mbinu ya barabara,Afya,kilimo,ufugaji na uwekezaji na kwamba miradi hiyo imeisababisha wilaya ya Chato kuendelea kuchanja mbuza za kimaendeleo.
Katibu mkuu wa Chama cha mpira wa miguu wilayani hapa,(CDFA) Mwl. Wilfred Machugu,amesema wametoa baraka zote za uendeshaji wa mashindano hayo baada ya kukidhi vigezo vinavyopaswa kutekelezwa kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.
Mashindano hayo yameandaliwa na mkuu wa wilaya hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wa michezo ikiwemo CRDB Bank,NMB Bank,Chato Beverage Co.Ltd na Rwaikondo Credit.