Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Katika hali isiyo kawaida kikongwe mmoja mwenye umri wa miaka zaidi ya 90, Hilda Ngasa mkazi wa Mtaa wa Kinyambwa Kata ya Kikuyu Mkoani Dodoma ameuawa kwa kukatwa mapanga na mwanaume mmoja aitwaye Yohana Luhanga ambaye anadhaniwa kuwa na ugonjwa wa afya ya akili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Martin Otieno, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa limetokea Julai Mosi Mwaka huu na kueleza kuwa mara baada ya kufanya shambulio hilo kijana huyo alishambuliwa na wananchi wenye hasira kali.

Akizungumza jana Julai 2,2023 amesema hiyo sio mara ya kwanza kwa mauwaji ya kikatili kutokea na kutumia nafasi hiyo kutoa wito kwa jamii kuepuka kujichukulia sheria mkononi.

Akizungumzia chanzo cha tukio hilo Kamanda Otieno amesema mtuhumiwa Yohana alienda kwa mama huyo kuomba kukata kuti ,lakini mama huyo ambaye ni marehemu alimwambia hawezi kukata mwenyewe atafute na watu wa kumsaidia na baada ya kujibiwa hivyo mtuhumiwa huyo alipata hasira na kuanza kumcharanga mama huyo hadi kupelekea kifo chake.

Mtuhumiwa Yohana Luhanga anayedaiwa kumuua kikongwe mwenye miaka zaidi ya 90 Hilda Ngasa.

Naye Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dokta Samweli Magesa ameeleza kuwa mnamo Julai 1 ,mwaka 2023 majira ya saa 6 mchana walipokea maiti moja na majeruhi mmoja aliyekuwa na umri wa zaidi ya miaka 30.

Amesema,”Katika uchunguzi wetu tuliofanya mwili huo ulikuwa na majeraha katika mwili wake ambapo ulisababisha na kukatwa na kitu chenye ncha kali katika maeneo mbalimbali”amesema.

Dk.Magesa pia ameeleza kuwa bibi huyo amepoteza uhai kutokana na kuvuja damu nyingi na kwamba mtuhumiwa wa mauaji hayo naye alipata majeraha katika maeneo mbalimbali ya mwili wake baada ya kupígwa na wananchi kama adhabu.

“Tulifanikiwa kumpa huduma ambazo zilitakiwa na tumemlaza wodini na kwa taarifa nilizonazo ni kwamba anaendelea vizuri lakini uchunguzi bado utaendelea kwa jinsi tutakavyokuwa tunaendelea kumuhudumia”amesema Dk.Magesa.

Kwa upande wa Mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni kutokana na kijana huyo kunyimwa kukata makuti ya mnazi pamoja na mboga za majani.
Sarah Kijaji amesema kuwa tukio hilo limeigusa jamii na kueleza kuwa mtuhumiwa wa mauaji hayo ana tatizo la afya ya akili.

“Huyu jamaa huwa ana ugonjwa na huwa anapita marà nyingi nyumbani kwa bibi huyo wakati akienda mjini ambapo mara nyingi alikuwa akimkuta akiwa na jembe lake analima kuna muda waliokuwa wanasalimiana vizuri,”amefafanua

Pamoja na hayo ameitahadharisha jamii kuwa makini na watu ambao hawako sawa kiakili Kwa kusaidia kuwapeleka kupata huduma za kitabibu kila inapobidi na kupunguza madhara.

Naye Petro Chibago ambaye ni mkazi wa eneo hilo amesema kuwa kijana huyo aliyefanya mauaji hayo huwa anatatizo la afya ya akiri ambapo huwa anaanguka kifafa na anafanya vitu vya kitofauti mtaani.

“Nilikuwa nimelala nikasikia makelele nilipotoka nje nikakutana na Yohana nikaamua kukimbia kwani Yohana anaogopeka,”amesema