Na James Mwanamyoto – OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde amesema Serikali haitomsamehe yeyote atakayebainika kukwamisha ujenzi wa miundombinu ya elimu katika shule za Sekondari na msingi.
Dkt. Msonde amesema hayo kwa nyakati tofauti akiwa wilayani Msalala, Ushetu na Kahama Manispaa kukagua utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya miundombinu ya shule za msingi na sekondari katika halmashauri hizo.
“Serikali haitomsahe yeyote atakayesababisha wanafunzi wakose mabweni na madarasa wakati imetoa kwa wakati fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo ya elimu,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Ili kuhakikisha miundombinu ya elimu inakamilika kwa wakati, Dkt. Msonde amezitaka menejimenti za halmashauri hizo kuongeza mafundi wenye uwezo wa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya elimu katika shule za sekondari na msingi ili wanafunzi wapate mazingira bora ya kupata elimu.
Ameongeza kuwa, ujenzi wa miundombinu hiyo ya elimu kupitia mradi wa BOOST ilikuwa imepewa muda maarumu wa kukamilika, hivyo amewataka viongozi wa halmashauri zote nchini kuhakiksha ndani ya siku 10 wanakamilisha miundombinu hiyo ili iweze kutumiwa na wanafunzi.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga ambaye ni Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga Bi. Dafroza Ndalichako amesema, ofisi yake itahakikisha watendaji wa halmashauri zote zinazoteleza Mradi wa BOOST katika eneo lake la utawala, wanafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya elimu.
…………………………….