Uongozi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) iliyopo jijini Arusha, unajitahidi kufanya kila linalowezekana kuficha vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka katika chuo hicho.
Hivi karibuni, uongozi huo umewasilisha serikalini kile kinachoonekana kuwa ni utetezi dhidi ya sehemu ndogo kati ya yale yaliyoandikwa na yanayokusudiwa kuandikwa na Gazeti la JAMHURI.
Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Burton Mwamila, amekwenda Baraza la Habari Tanzania, ikiwa ni juhudi zake binafsi na wasaidizi wake katika kuficha ukweli wa yale yanayoendelea katika NM-AIST.
Wakati shauri hilo katika Baraza la Habari likiwa bado linaendelea na taratibu zake, ni vema wasomaji wakajua kinachoendelea katika chuo hiki.
Fedha za utafiti za wanafunzi
Fedha za utafiti za wanafunzi ni miongoni mwa fedha zinazodaiwa kutumika vibaya. Kuna udanganyifu kwenye bajeti zinazowasilishwa kwenye vikao vya chuo na fedha halisi wanazopewa wanafunzi.
Wanafunzi wa Shahada ya Uzamivu wanapewa malazi (accommodation) ya hali ya chini tofauti na kiwango kilichotolewa na mfadhili.
Kuna udanganyifu na kupandisha bei kwenye ununuzi wa vifaa vya utafiti wa wanafunzi.
Wanafunzi wajawazito walikuwa wakiondolewa kwenye hosteli za chuo kwa lazima pasipo kurudishiwa fedha zao, licha ya kuwa zimelipwa na mfadhili.
Wanafunzi wanalazimishwa kuzalisha vitabu vya utafiti kwa fedha zao, licha ya kuwa chuo kimechukua fedha hizo kutoka kwenye ada na chuo kilipaswa kuzalisha. Wanafunzi waliohitimu mwaka 2013 vitabu vyao havipo kwenye kumbukumbu za maktaba kwa sababu fedha za kuzalisha zilizolipwa kwenye ada zilitumika kwa mambo mengine.
Chuo hakirejeshi fedha za tahadhari (caution money) za wanafunzi hata kama wamefanya uhakiki wa kutokudaiwa au kuharibu mali yoyote.
Chuo hiki kina wanafunzi wa aina nne:
A: Wanafunzi wanaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania moja kwa moja
Ufadhili wa wanafunzi hawa ulitokana na uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Nne ambako iliamuriwa wanafunzi wanaosoma chuoni hapo, wapewe ufadhili wa Serikali hadi hapo chuo kitakapoweza kujisimamia chenyewe. Ufadhili huu ulianza mwaka 2011 na Serikali iliufuta mwaka 2013.
Wanafunzi walio chini ya ufadhili huu kwa sasa ni wa mwaka wa tatu wa Shahada ya Uzamivu.
B: Wanafunzi wanaofadhiliwa na Kamisheni ya Sayansi (COSTECH):
Wanafunzi hawa fedha zao za ufadhili zinatoka Costech na kwa utaratibu wao fedha za ufadhili huwa zinapelekwa chuo husika na chuo huwapatia wanafunzi fedha zao, hasa zile wanazopaswa kupewa moja kwa moja. Mfano fedha za kujikimu na utafiti.
C: Wanafunzi wanaofadhiliwa na Bodi ya Mikopo:
Huu ni utaratibu mpya ambao umeanza miaka miwili iliyopita baada ya Serikali kuondoa ufadhili wa moja kwa moja.
D: Wanafunzi wanaofadhiliwa na miradi, mashirika, waajiri na wengineo:
Kabla ya mabadiliko yamuundo wa ada (fee structure) mwaka jana, chuo kilikuwa kinalazimisha fedha zote zikiwamo za utafiti, malazi na za kujikimu ziingizwe chuoni na baada ya hapo ndipo wanafunzi wapewe. Utaratibu huu ndiyo uliozaa madudu mengi ambako wanafunzi wamekuwa hawapewi stahiki zao kama inavyostahili. Hapa ndiko kwenye jipu lenyewe.
Tukianza na fedha za utafiti
Kabla ya mabadiliko ya fee structure, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu alikuwa analipiwa Sh milioni 37.5 na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili alikuwa analipiwa Sh milioni 12.5 kwa ajili ya utafiti.
Ushahidi uliopo kwenye mafaili ya wanafunzi unaonesha kuwa wapo ambao wamepewa chini ya Sh milioni 2 kati ya milioni 37.5 kufanya utafiti kwenye Uzamivu; na kuna ambao wamepewa chini ya Sh milioni 1 kufanya utafiti kwenye Shahada ya Uzamili.
Chuo kimekuwa kikitumia njia mbalimbali kuhakikisha hakitoi fedha kwa wanafunzi ikiwamo kutumia kisingizio cha Sheria ya Ununuzi wa Umma ili kuwabana wanafunzi. Sheria hii imekuwa ikitumika kulazimisha chuo ndicho kiwe mnunuzi mkuu wa mahitaji yote ya wanafunzi.
Kwa mfano, kwa kushirikiana na wazabuni waliopo Arusha ambao majina yao tunayahifadhi kwa sasa, chuo kimekuwa kikinua kemikali na vifaa vingine kwa bei ambazo wakati mwingine ni mara tatu au zaidi ya bei za soko.
Kulipa fedha za kujikimu Sh 50,000 kwa siku kwa wanafunzi watakaokuwa wanafanya utafiti nje ya Arusha. Kiwango hiki hakipo kabisa kwenye viwango vya malipo ya Serikali, lakini chuo kimekuwa kikilazimisha kuwalipa wanafunzi kiwango hicho.
Chuo kimekuwa kililazimisha wanafunzi wafanye utafiti Arusha ili kisilipe hizo wanazoziita fedha za kujikimu.
Chuo kimeweka siku 14 hadi 90 tu kwa wanafunzi watakaoruhusiwa kufanya utafiti wao nje ya Arusha.
Kwa wanafunzi wanaosoma Hisabati na Kompyuta wamekuwa wakishinikizwa waandae utafiti ambao kimsingi wanapaswa waufanyie chuoni na hivyo kupewa kiwango kidogo cha fedha.
Miongoni mwa waliohitimu kuna ambao hawakupewa fedha kabisa na kuna mmoja ambaye amemaliza mwaka 2015 na mahafali yake yamefanyika Aprili, mwaka huu aliyepewa Sh milioni 1.3 tu kati ya Sh milioni 37. Ushaidi wa haya yote unapatikana kwenye mafaili ya wanafunzi. Tunaomba haya uongozi wa chuo uyaweke wazi kwa Waziri Mkuu au katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Mbinu hii ilianza tangu chuo kilipofunguliwa bila kujali aina ya ufadhili wa wanafunzi.
Hata wanafunzi wanaofadhiliwa na mashirika ya kimataifa ambao malipo yao yamekuwa yakitolewa kwa fedha za kigeni, wanafunzi wamekuwa wakilipwa kwa shilingi (za Tanzania) na kwa viwango visivyowiana na thamani ya fedha.
Mfano mzuri wa haya ni wa wanafunzi wa mwaka wa tatu wa Shahada ya Uzamivu na wale wa Shahada ya Uzamili waliofanyiwa mahafali Aprili wanaofadhiliwa na Serikali moja kwa moja.
Chuo kiliwaambia Serikali imetoa Sh milioni 4 hadi Sh milioni 6 tu kwa ajili ya wao kufanya utafiti. Muda wote ambao wamekuwa wakiomba uthibitisho wa mabadiliko ya mkataba, chuo hakiko tayari kujibu kwa maandishi zaidi ya kuomba vikao nao na kuwajibu kwa mdomo tu kuwa Serikali haijapeleka fedha.
Pamoja na kuambiwa uwepo wa kiasi kidogo hicho cha fedha, bado chuo kimetoa fedha chini ya Sh milioni 1 kwa baadhi ya wanafunzi waliomaliza Shahada ya Uzamili na wengine wanaoendelea na Shahada ya Uzamivu.
Hata wanafunzi wanaofadhiliwa na Costech wapo waliopewa chini ya Sh milioni 1 kati ya Sh milioni 12.5 zilizotewa na Costech kwa ajili ya mwaka wa kwanza wa utafiti. Wakati huo huo chuo kinawataka wanafunzi hao waiandikie Costech kuomba fedha zilizobaki.
Kwa sasa hali ni mbaya na kuna uwezekano utafiti ukafanyika chini ya kiwango, ingawa hili linaweza lisiwe ni tatizo kwa uongozi wa chuo, kwa kuwa dalili zote zinaonesha viongozi wa chuo wanathamini fedha kuliko ubora wa elimu.
Gharama za malazi
Chuo cha Mandela kimekuwa kikiwatoza wafadhili wa wanafunzi wa Shahada ya Uzamivu Sh 390,000 kwa mwezi kwa maelezo kwamba wanaishi kwenye nyumba za chuo zinazoitwa ‘PhD Villages’. Kinyume chake, chuo kilitoa nyumba hizo kwa PhD waliongia mwaka 2011 pekee. Waliobaki waliwekwa kwenye vyumba vya wanafunzi wa Uzamili vyenye thamani ya Sh 150,000 tu kwa mwezi. PhD Villages kwa sasa zina miaka miwili hazikaliwi na watu na zinaharibika tu.
Katika suala hili la malazi, Uongozi wa Chuo ulikuwa na utaratibu wa kuwaondoa kwenye mabweni wanafunzi wajawazito hasa wale wa Shahada ya Uzamili bila kuwarudishia fedha walizolipiwa na wafadhili wao. Utaratibu huu uliachwa baada ya malalamiko kutoka kwa wanafunzi.
Profesa Mwamila ajibu maswali haya
Wakati Uongozi wa Chuo chini ya Profesa Mwamila, ukifanya juhudi kubwa kujitetea, ni vema ukatoa majibu kwa hoja hizi:
1: Profesa Dunstan Shemmwetta aliondoka katika ajira ya Chuo cha Mandela na kuondoka katika nyumba iliyokodiwa Machi, 2013. Profesa Mwamila anapaswa ajibu maswali yafutayo:
(a) Kati ya Aprili 2013 hadi Desemba 2013 akina nani walikuwa wanaishi katika nyumba hiyo?
(b) Kati ya Januari 2014 hadi Desemba 2014 kina nani walikuwa wakiishi katika nyumba hiyo?
(c) Kati ya Januari 2015 hadi Desemba 2015 ni kina nani walikuwa wanaishi katika nyumba hiyo?
(d) Kati ya Januari 2016 hadi sasa ni nani alikuwa akiishi katika nyumba hiyo?
2: (a) Kwa nini Profesa Mwamila asiweke hadharani mikataba ya wageni anaosema waliwahi kuishi katika nyumba hiyo, au anaotaka wakae katika nyumba hiyo? Je, ni wajibu wa chuo kuwalipia nyumba?
(b) Tangu Chuo cha Mandela kianzishwe rasmi mwaka 2011 kwa intake ya kwanza, Research Village, nyumba za wageni na zile nyumba zilizopo chuoni kwa ajili ya wafanyakazi hazijawahi kujaa; sasa iweje akodishe nyumba nje ya chuo kwa fedha nyingi? Kwanini atumie mamilioni ya shilingi kulipa nyumba inayosubiri wageni?
3: (a) Profesa Mwamila anataka kueleza kuwa Baraza la Uongozi la Chuo liko juu ya Serikali, kwa hiyo nyaraka za maagizo ya Serikali hazipaswi kuheshimiwa?
(b) Profesa Mwamila anaweza kuthibitisha kuwa Baraza la Uongozi la Chuo lina mamlaka ya kubatilisha nyaraka na miongozo ya Serikali?
(c)Profesa Mwamila anaweza kueleza ni wapi Baraza la Uongozi la Chuo limepata mamlaka ya kubatilisha nyaraka za Serikali?
(d) Ni kikao gani cha Baraza la Uongozi wa Chuo kiliamua kubatilisha maelekezo ya Serikali?
4: Ni wahadhiri wangapi na kwa majina yao, walikwenda kufundisha Chuo cha Mandela kwa muda na wakapewa nyumba za chuo kuishi? Wahadhiri wanaofundisha kwa muda huwa wanaishi wapi?
5. Mfanyakazi wa chuo ambaye alikuwa akiendesha gari la mkuu wa chuo, tangu aache kuendesha gari hilo; haendeshi gari lolote la chuo ingawa analipwa mshahara na Hazina.
Kwa miaka miwili amekuwa akifanya kazi katika mradi wa VRILOUS baada ya mradi huo kutangaza nafasi ya kazi, naye akapata nafasi hiyo, na analipwa mshahara huko. Ana mishahara miwili. Profesa Mwamila, ajibu maswali haya.