Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amesema watanzania wana kila sababu ya kumpa maua Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi nzuri aliyofanya katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake.
Aidha ,amekemea tabia ya baadhi ya watu wanaoita wenzao chawa kisa wamepongeza utendaji kazi wa Rais Samia na kusema hata Biblia imeandika kwamba moyo usio na shukrani hukausha mema yote.
Akichangia mjadala wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2023/2024, Juni 21,2023,Mtaturu amesema katika uongozi wake kazi kubwa ameifanya ikiwemo kudumisha demokrasia nchini,kuweka uwazi wa serikali,diplomasia na kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo wanajivunia.
“Kwa niaba ya wananchi wa Singida Mashariki walionipigia kura nyingi sana,natamka hadharani kumpongeza Mh Rais Samia kwa kazi kubwa aliyoifanya katika muda wa miaka miwili, hakika kazi nzuri anayofanya anastahili kupewa maua yake ya kutosha,kwa hakika wale wenye nia njema hawatasita kumpa maua yake,tumpe maua mengi Mh Rais kwa kazi njema anayoifanya,”amesema.
Mtaturu amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu nchini kutotaka watu kupongezana kwa mambo mazuri yanayofanyika jambo ambalo sio sawa.
“Wengi wamefika mahali wanasema ukimpongeza unakuwa wewe ni chawa ,Mh Mwenyekiti hata kwenyeBbiblia imeandikwa kwamba moyo usio na shukrani hukausha mema yote,kwa hiyo watanzania mtu akifanya jambo zuri mpongeze ili afanye kazi zaidi,kwa hiyo Rais anapofanya kazi nzuri uungwana wa kawaida unatakiwa umpongeze kwa sababu amefanya kazi nzuri ,”ameongeza.
Akitolea mfano jimboni kwake kazi nzuri iliyofanyika Mtaturu amesema,Wilaya ya Ikungi kwa ujumla imepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 7 ili kutekeleza miradi ya maendeleo na hiyo inaonyesha kuwa fedha nyingi zimeshuka kutekeleza miradi.
“Tunajivunia sana uongozi wa Rais wetu,tunajivunia kiongozi wetu anapofanya vizuri,kuna maeneo yalikuwa hayana madarasa leo madarasa yapo,kuna maeneo kulikuwa hakuna vituo vya afya leo kuna vituo vya afya,kuna maeneo barabara zilikuwa zimejifunga sasa zimefunguliwa,leo wilaya yetu ya Ikungi tulikuwa hatujawahi kuona lami sasa lami inawekwa,tulikuwa gizani hakuna taa barabarani,tulikuwa tunalala mapema lakini leo hii taa za barabarani zinawekwa,tutakuwa watu wa ajabu kabisa bila ya kumpongeza Rais na kuishukuru serikali.
“Lakini mzee Mkapa alisema kushukuru ni kuomba tena ,tunaamini tunaposhukuru tunamuomba tena Rais atuletee fedha tuweze kuleta maendeleo zaidi ya wananchi,”ameongeza.
Ametumia nafasi hiyo kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba kwa kazi nzuri ya kusimamia miradi ya maendeleo na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Thomas Apson na Mkurugenzi wa Ikungi Justice Kijaz kwa kazi nzuri ya kusimamia maendeleo na usimamizi wa mapato uliopelekea Halmashauri kupata hati safi.