Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya kugharamia huduma za upasuaji na matibabu ya ubingwa bobezi ili kurahisha upatikanaji wa huduma hizo kwa Watanzania wenye hali zote.
Waziri Ummy amesema hayo kwenye ufunguzi wa Kongamano la 28 na Mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji nchini Tanzania unaofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.
“Huduma hizo za upasuaji na matibabu ya ubingwa bobezi zitapatikana hapa hapa kwetu Tanzania, kwa mfano hospitali ya Benjamini Mkapa walivyofanya katika upandikizaji wa ULOTO ambao umegharimu shilingi milioni 58, na Serikali imetenga Bilioni 5 ambapo tunaweza kupata wagonjwa 100” amesema.
Aidha, Waziri Ummy amesema, Serikali inaanza mchakato wa kuwasambaza upya Madaktari Bingwa nchini ili kutatua changamoto ya uhaba wa madaktari hao katika maeneo yenye uhitaji mkubwa Mikoani.
“Lakini pia sisi kama Serikali tutajitahidi kuboresha maslahi yenu (Madaktari Bingwa wa Mifupa) na maslahi ya wafanyakazi wengine katika vituo va kutolea huduma za afya nchini” ameongeza Waziri Ummy.
Pia, Waziri Ummy amezitaka hospital za Muhimbili, MOI, JKCI na Mloganzira kutoajiri madaktari moja kwa moja kutoka vyuoni bali wawachukue walio mikoani ambao wamekuwa na uzoefu wa muda mrefu katika utoaji huduma.
“Nimeshapeleka mapendekezo haya kwa wenzetu wa utumishi kwamba (Muhimbili, MOI, JKCI na Mloganzira) wasiajiri madaktari mojo kwa moja kutoka vyuoni bali wawachukue walio Mikoani ambao wamekuwa na uzoefu wa muda mrefu na hawa wapya ndio tuwapeleke Mikoani” amesema Waziri Ummy.
Amesema,nchi yetu bado inauhitaji mkubwa wa Madaktari Bingwa na Ubingwa Bobezi ikiwemo Madaktari wa Upasuaji, hivyo Serikali itaendelea kutenga fedha ili kusomesha Wataalam wengi zaidi katika ngazi ya Ubingwa na Ubingwa bobezi.
Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya inatambua uwepo wa changamoto ya fedha za matibabu kwa Watananzia ndio maana tumekuja na swala la Bima ya Afya kwa Wote (NHIF).
“Tunatambua matibabu yamekuwa na gharama hivyo Bima ya Afya kwa Wote ndio itawezesha Watanzania kupata huduma kwa urahisi ndio maana tupo tunaendelea na mchakato wa kupitishwa” amesema Waziri Ummy.
Sambamba na hilo, Waziri Ummy amesema, Serikali iko tayari kuyapokea na kuyafanyia kazi maazimio yatakayotokana na kikao hiki ambayo naamini yatakuwa yenye malengo mahususi kwaajili ya uboreshaji katika Sekta ya afya.
Kauli mbiu ya Kongamano hilo la 28 na Mkutano Mkuu huo wa mwaka huu inasema “KUJENGA MFUMO WA UTOAJI HUDUMA ZA UPASUAJI MADHUBUTI, UNAOFIKIKA NA WENYE CHARAMA NAFUU TANZANIA