Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema miradi ya vitega uchumi inayofanywa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) itaongeza tija kwenye Mfuko.
Amesema hayo Juni 14, 2023 wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa hoteli ya kitalii ya nyota tano inayomilikiwa na NSSF iliyopo katika eneo la Capripoint jijini Mwanza.
Rais Dkt. Samia ameipongeza NSSF kwa mradi wa hoteli hiyo kuwa ni kitu kizuri ambapo itakapokamilika itachochea sekta ya utalii na kuongeza tija kwenye Mfuko.
“Hongereni sana NSSF kwa kweli mradi huu ni kitu kizuri ,” amesema Rais Dkt. Samia.
Alisema anaamini kuwa wataalamu wameshapiga mahesabu kuwa mradi huo utakuwa na tija kwa NSSF na Taifa kwa ujumla, na kwamba Mfuko ukipata mapato mengi zaidi uangalie na maeneo mengine ya kuwekeza kama vile Dodoma.
Mhe. Rais Dkt. Samia aliwaomba wafanyakazi wa NSSF kuendelea kutoa huduma bora na kuchunga fedha za wanachama ili wanapostaafu waweze kulipwa mafao yao mara moja.
Naye, Protobas Katambi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, alisema Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inawekeza kwa lengo la kulinda thamani ya michango ya wanachama na kuahidi kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaendelea kushirikiana na Mfuko katika kuangalia maeneo mengine ya uwekezaji.
Akitoa maelezo ya mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Msomba alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2024.
Mshomba alisema kukamilika kwa hoteli hiyo kutachangia shughuli za kiuchumi katika jiji la Mwanza ukizingatia kuwa jiji hilo linashughuli nyingi za kiuchumi ikiwemo uvuvi na madini.
Alisema ujenzi wa hoteli hiyo ni vema ukaenda sambamba na uendelezaji wa uwanja wa ndege wa Mwanza kwa sababu watu watakao kuja kwa ajili ya utalii watahitaji kulala katika hoteli hiyo hasa ukizingatia kuwa umbali wa kutoka Mwanza hadi Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni takribani kilomita 140.
Akitoa maelezo ya hoteli hiyo, Mhandisi Helmes Pantaleo ambaye ni Meneja Usimamizi wa Miradi wa NSSF, alisema hoteli hiyo ina jumla ya ghorofa 16, vyumba 168 vya kulala vya aina mbalimbali ikijumuisha sehemu ya kupumzikia Rais (Presidential Suite), migahawa, sehemu za vinywaji na michezo (sports bar).
Pia, kuna ukumbi mkubwa wa mikutano wa kuchukua watu 500, kumbi ndogondogo za mikutano, bwawa la kuogelea, sehemu za kufanyia mazoezi, ofisi, maduka, sehemu ya maegesho ya magari na juu kabisa ya jengo hili kuna sehemu ya kutua chopa (helkopta).
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza mara baada ya kupokea maelezo kuhusu ujenzi wa hoteli ya kitalii ya nyota tano inayomilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambapo alipongeza NSSF kwa mradi wa hoteli hiyo.