Na Dotto Kwilasa, JamhiriMedia, Dodoma.
Serikali imetia saini mkataba wa Mradi Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam(DMDP) awamu ya pili na wakandarasi watatu wenye thamani ya shilingi Bilioni 800 huku ikiahidi kusimamia mradi huo ili kama kuna dosari zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza zisijirudie.
Wakandarasi hao ni Mhandisi Consultancy LTD & Luphan ambaye atasimamia Wilaya ya Temeke na Kigamboni, Nimeta Consultancy LTD atakayesimamia Kinondoni na Ubungo na UWP Consultancy LTD atakayesimamia Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini leo Mei 30,2023 Jijini Dodoma Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Angellah Kairuki amesema anaamini kupitia mradi huo changamoto nyingi zitatatuliwa.
Ametaja changamoto hizo kuwa ni ujenzi holela wa makazi, miundombinu duni ya usafiri, mabadiliko ya tabia nchi kwa jiji la Dar es Salaam zinazosababisha mafuriko na utupaji taka ngumu hovyo.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dokta Mwigulu Nchemba amesema ujio wa mradi huo umeleta faraja kwa wabunge wa Dar es salaam ambao wamekuwa wakiuzungumzia mara kwa mara.
Akitoa taarifa ya mradi, Mratibu wa miradi ya Serikali kupitia mikopo ya Benki ya Dunia, Tamisemi na Tarura, Mhandisi Humphrey Kanyenye amesema jiji la Dar es Salaam lina changamoto ya usanifu, utunzaji taka ngumu, mafuriko na miundombinu isiyokidhi hivyo mradi huo unaenda kuziondoa.
Naye Mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Dar es salaam Faustine Ndugulile ameishukuru serikali kwa utekelezaji wa mradi huo na kutoa angalizo kwamba wao kama wawakilishi wa wananchi watasimama kidete kuhakikisha unafanikiwa.
Mwenyekiti huyo amesema kwa Mkoa wa Dar Es Salaam Kipaumbele cha kwanza ni barabara cha pili barabara na cha tatu ni barabara na kufafanua kuwa hali hiyo inadhihirisha wazi kuwa wananchi wanahitaji barabara kabla ya mambo mengine.
Amesema Mkoa huo unapaswa kupewa kipaumbele hasa Kutokana na mchango wake kwenye masuala ya uchumi wa nchi.
“Lazima tuupe kipaumbele Mkoa huu,barabara zake hazilingani na mchango wake kwenye uchumi,tunataka Jiji la hili liwe na muundo na uendeshaji tofauti na mikoa mingine, tunatambua barabara ni maisha , barabara ni uchumi,”amesema
Utekelezaji wa mradi huo utaanza April mwaka 2024 ambapo asilimia 74 ya fedha zitatumika kukarabati barabara, mifereji, maeneo ya wazi, masoko, vituo vya mabasi, kurekebisha miundombinu ya taka ngumu, kujenga uwezo kwa halmashauri hizo.