Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Serikali imeeleza kuwa Mpango wa Hiari wa Afrika wa Kujitathmini katika Masuala ya Demokrasia na Utawala Bora (APRM) nchini Tanzania imekamilisha taratibu za kuwasilisha Ripoti ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa APRM (2014 – 2029) kwenye Kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja wa Afrika wanaoshiriki katika Mpango wa APRM kitakachofanyika mwanzoni mwa mwaka 2024.

Akizungumza leo Mei 30, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax alisema kuwa Mpango wa Hiari wa Afrika wa Kujitathmini katika Masuala ya Demokrasia na Utawala Bora (APRM) ni Wakala Maalum wa Umoja wa Afrika ulioanzishwa mwaka 2003 kwa lengo la kufanya tathmini za mara kwa mara za utawala bora zenye nia ya kuimarisha maeneo ambayo nchi inafanya vizuri, kuibua changamoto za utawala bora, na kutoa mapendekezo ya ufumbuzi wa changamoto.

“Ripoti imeangazia maeneo manne ya tathmini ambayo ni Siasa na Demokrasia, Usimamizi wa Uchumi, Utendaji wa Mashirika ya Biashara na Maendeleo ya Jamii. Ripoti hiyo ina maelezo yaliyofanyiwa utafiti kwa kipindi cha mwaka 2014 hadi 2019. Maandalizi ya Ripoti pia yamezingatia miongozo na kanuni za APRM”, ameeleza Dkt. Tax.

Amefafanua muhtasari wa maudhui ya kila eneo la tathmini ambapo katika eneo la Siasa na Demokrasia, Ripoti inaonesha kuwa hatua zimepigwa katika kutatua changamoto kwenye maeneo yote ya tathmini ikiwa ni pamoja na suala la utatuzi wa migogoro, kufanyiwa kazi kwa maeneo sita ya Muungano, mageuzi makubwa katika utumishi wa umma sanjari na uimarishaji wa taasisi zilizopewa jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa yanaifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano.

Pia, haki za makundi ya wanawake, watoto, vijana na wakimbizi zimeendelea kulindwa kwa kuwekewa sera rafiki zinazosimamia maslahi mapana ya makundi hayo.

“Kuhusu usimamizi wa uchumi, nchi yetu imeendelea kutekeleza sera za uchumi mpana zinazolenga kupata maendeleo endelevu. Pia, katika eneo la Usimamizi wa Mashirika ya Biashara Serikali imejielekeza katika kuimarisha mifumo ya udhibiti wa mashirika ya biashara utakaowezesha kupatikana kwa maendeleo endelevu” amesema Dkt. Tax.

Aidha, kwa upande wa maendeleo ya jamii Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha ukusanyaji wa kodi kwa lengo la kuwa na uwezo wa kujitegemea na kuimarisha utoaji wa huduma mbalimbali za jamii.

Mwezi Februari 2023, APRM Tanzania ilishiriki kikao cha Wakuu wa Nchi Wanachama wa Mpango wa APRM kilichofanyika kwa njia ya mtandao. Katika mkutano huo, Muungano wa Visiwa vya Comoro ilijiunga na Mpango wa APRM na kuwa mwanachama wa 42.