Na Mwandishi Wetu, Jamhuri Media
Mwanasiasa Mkongwe Tanzania ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Mazishi, Stephen Wasira ameeleza namna Nimrod Mkono alivyojitoa kwa hali na mali hata kutumia pesa zake kuwasaidia wananchi enzi za uhai wake.
Wasira ameeleza hayo leo Mei 27, 2023 jijini Dar es Salaam na kusema kusema kuwa, Mkono alitumia rasilimali zake binafsi katika kutatua matatizo ya wananchi jimboni kwake hata pale msaada wa serikali ulipochelewa ili kusaidi maendeleo ya watu.
“Moyo wa kusaidia jamii ulikuwa mkubwa sana, kwa kutumia rasilimali zake na siyo kwamba yeye alikuwa Tajiri kuliko matajiri wengine. Amejenga ‘High School’ halafu akazikabidhi kwa serikali” amesema Wasira.
Naye aliyewahi kuwa mbunge wa Chadema katika jimbo la Musoma Mjini Vincent Nyerere 2010 hadi 2015 ameelezea kuwa Nimrod Mkono alimpa ushauri na msaada wa kisheria kuhusu mambo mbalimbali bungeni, pia namna alivyoshirikiana naye katika shughuli za kimaendeleo na miundombinu alipokuwa mbunge pasina kujali tofauti za vyama
Vyao.
“Kwa mfano Miundombinu ya Musoma mjini haikuwa mizuri sana lakini aliniambia iko namna ambayo ninaweza kukusaidia kuishauri serikali ihamishe miradi ya barabara ambazo haziwezi kutengenezwa halimashauri, zipelekwe TANROADS bila kuvunja sheria na ilifanikiwa.’
Aidha Nyerere ameeleza kuwa Mkono alikuwa na mapenzi makubwa sana na elimu na alikuwa akimsihi sana kusisitiza juu elimu katika michango take bungeni ili kuhakikisha watu wa Mkoa wa Mara wanapata elimu.
Mkono aliye wahi kuwa mbunge wa Msoma vijjini na Butiama kwa Miaka 15 na kisha kuwa Mbunge wa Butiama kwa miaka 05 kupitia (CCM) alifariki Dunia April 18, 2023 nchini Marekani alikokuwa akipewa matibabu tangu mwaka 2018.
Mwili wake umewasili leo Mei 27, 2023 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kupelekwa nyumbani kwake Masaki jijini Dar es salaam kwa ajili ya ibaada.
lbada rasmi ya kuaga mwili huo inatarajiwa kufanyika Jumapili Mei 28, 2023 Ukumbi wa Karmjee , ambapo imeelezwa kuwa itaongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Samia kisha utasafirishwa kuelekea Mwanza hadi kijini kwao Busegwe Butiama Mkoani Mara kwa ajli yaa mazishi.