Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU)Mkoa wa Dodoma katika utekelezaji wa majukumu yake imepokea jumla ya malalamiko 138 ambapo kati yake, malalamiko 81 yalihusu rushwa na mengine 7 taarifa zake kuhamishiwa Idara nyingine kwa hatua zaidi.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma John Joseph amesema hayo leo Mei 26,2023 wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu ufuatiliaji utekelezaji wa miradi 36 ya maendeleo ya zaidi ya bilioni 16.8 ikiwa ni sehemu ya Utaratibu wake wa kutoa taarifa kwa kila kipindi cha miezi mitatu.

Amesema malalamiko 57 yalihusu rushwa ambapo yalipelekwa kufunguliwa majalada ya uchunguzi na kati ya hayo uchunguzi wa majalada 17 umekamilika ,mashauri mawili yamefunguliwa mahakamani na mengine 15 hatua mbalimbali za kisheria zinatarajiwa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa.

Mkuu huyo wa TAKUKURU amefafanua kuwa Idara zinazo lalamikiwa Kutokana na taarifa 57 ni pamoja na Elimu (11), TAMISEMI (9),Sekta binafsi (9), Ardhi (7),Afya (7), Polisi(5), Kilimo(3),Manunuzi (2), Mahakama (1), Maji (1), Mazingira (1)na fedha (1).

“Mashauri mapya manne yametolewa maamuzi ambapo hadi sasa mawili tumeshinda na mawili tumeshindwa ,aidha jumla ya mashauri 31 yanaendelea kusikilizwa mkoani Dodoma na yako katika hatua mbalimbali,”amesema

Pamoja na hayo amesema katika kipindi cha miezi mitatu TAKUKURU Mkoa wa Dodoma wamefanya kazi za uzuiaji rushwa,uelimishaji wa jamii na uchunguzi.

Amefafanua kuwa katika jukumu la uzuiaji rushwa wamefanya tafiti 10 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma kwa Wilaya za Dodoma, Chamwino na Chemba na kufanya tafiti moja moja kwa kila Wilaya.

“Kwa Wilaya ya Bahi zilifanyika tafiti mbili na katika Wilaya ya Kongwa zilifanyika tafiti tano,tumeweza kufanya warsha tano ambazo zilitumika kuwasilisha matokeo ya chambuzi za mifumo zilizofanyika Kwa lengo la kushirikisha jamii kutafuta ufumbuzi dhidi ya mianya ya rushwa,”amefafanua.

Katika ufuatiliaji wa utejekezwaji miradi ya maendeleo, TAKUKURU Mkoa wa Dodoma imefuatilia miradi 36 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 16 ambayo inatoka sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, Ardhi, Kilimo, ujenzi, barabara na fedha .

Kwa mujibu wa Mkuu wa TAKUKURU Dodoma jumla ya miradi 22 ya elimu imefanyiwa ufuatiliaji, Kilimo miradi 5,fedha 3 na afya miradi 4 hali iliyosaidia kufikia fedha kiasi cha shilingi 1,050,000 katika Wilaya ya Chamwino.

“Miradi 21 imetolewa ushauri na elimu pia ufuatiliaji unaendelea, miradi 7 imekamilika ,miwili imetolewa maelekezo, chambuzi za mifumo ya warsha miradi miwili,miradi miwili inaendelea na ufuatiliaji nyaraka katika Wilaya ya Chamwino,”ameeleza