Na WMJJWM, Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amelitaka Baraza la Ushauri la Wazee kuzingatia malengo ya Baraza hilo ambalo ni kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu na kuweka mikakati ya kutatua changamoto zinazo wakabili ili kuchochea maadili mema, uzalendo na ushiriki katika shughuli za ustawi na maendeleo ya jamii nchini.
Waziri Dkt. Gwajima amesema hayo alipokuwa akifungua Kikao cha Baraza la wazee taifa kilichofanyika jijini Dodoma ambapo amesema Serikali itaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na Mabaraza hayo katika ngazi zote.
“Tumeendelea kushirikisha Baraza la Wazee katika kufanya ufuatiliaji wa huduma mbalimbali na miradi ya ustawi wa jamii katika maeneo mbalimbali ikiwemo vituo vya Ustawi wa Jamii kushirikisha Baraza la Wazee kwenye Vikao na Mafunzo mbalimbali yanayoratibiwa na Wizara (Afya ya Akili na Msaada wa Kisaikolojia)” amesema Dkt Gwajima.
Waziri Dkt. Gwajima amekumbusha pia wajibu wa wazee katika jamii hususani suala la maadili kwamba ni wakati wa kurejesha mifumo ya asili yenye kuchochea maadili mema katika jamii kwa sababu limekuwa ni changamoto.
“Wazee tumikeni kikamilifu kukemea yale yote yanayosababisha ukatili, unyanyasaji, unyanyapaa, mauaji katika jamii pamoja na mmomonyoko wa maadili ambao unataka kuliangamiza Taifa” amesema Dkt. Gwajima.
Pia Waziri Dkt. Gwajima amesema Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuendelea kuboresha huduma kwa wazee ambapo eneo la Afya limepewa kipaumbele hasa vitambulisho vya matibabu bure (ICHF) kwa wazee wasiojiweza ambapo kuanzia Julai, 2022 hadi Aprili, 2023 wazee 2,117,637 wametambuliwa katika Mikoa 26 ambapo Wazee 585,672 sawa na asilimia 27.65 walithibitishwa hawajiwezi na wamepatiwa vitambulisho hivyo.
Katika hatua nyingine Waziri Dkt. Gwajima amewakumbusha wajumbe wa baraza hilo na jamii kwa ujumla kuhusu siku ya kupinga Ukatili dhidi ya Wazee tarehe 15 Juni, na kaulimbiu yake, “Wazee wanastahili heshima na usikivu Wetu” na kuwaomba viongozi wote wa mikoa na wadau kuyapa uzito maadhimisho hayo kwa kuhakikisha kuwa kila mkoa unashiriki kikamilifu kujenga uelewa kwa jamii juu ya haki, ulinzi na usalama kwa wazee.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa Lameck Sendo akizungumza kwa niaba ya wazee ameomba suala la huduma za afya lishugulikiwe ili liwasaidie wazee kupata huduma sahihi na kwa wakati pale wanapopata matatizo.
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Maxmillian Kwangu akielezea mkakati wa huduma za Wazee amesema tayari taratibu za Madirisha ya wazee zimeshaanza kuwekwa na maeneo mengine madirisha hayo yanafanya kazi hususani kwenye vituo vya afya kwa lengo la kuwasaidia wazee kupata huduma ya afya.