Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amefanya ziara ya kustukiza katika soko la Mwenge ili kujionea hali halisi ya kinachozungumzwa na kulalamikiwa na wafanyabiashara.
Ziara ni ya kwanza baada ya kuhamishwa kituo cha kazi na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kutoka Mkoa wa Kagera.
Amesema kuwa ipo haja ya kusikia wafanyabiashara wanasema nini na kuanza kufanyiwa kazi changamoto zinazowakabili.
“Pamoja na kuwa sijaingia ofisini rasmi lakini nimeona ipo haja ya kusikia hasa huku mtaani watu wanasema nini, lakini katika moja eneo nililopita watu wanalalamikia uwepo wa kodi kubwa zisizoweza kulipwa na wafanyabiashara kutokana na kiwango kikubwa cha VAT ambayo ni asilimia 18” amesema Chalamila.
Aidha amesema suala lingine ambalo linalalamikiwa na wafanyabiashara hao ni kuhusiana na idara ya forodha ambayo imeweka viwango vikubwa vya kodi hasa katika vitenge pamoja na mlolongo mrefu wa ufuatiliaji ambapo ni kikwazo kwa wafanyabiashara wengi.
“Jambo la tatu ambalo nimelisikia ni kuwepo kwa zoezi la kamata kamata kwa wafanyabiashara Kariakoo na kuwakosesha uhuru pamoja na kuleta usumbufu kwa wateja wao na hasa kwa wateja kutoka Kongo, Zambia, Malawi pamoja na mataifa mengine,” amesema Chalamila.