SERIKALI ya Tanzania imejipanga kuendelea kunufaika na fursa zinazotokana na Mtangamano wa Kikanda ili kuwawezesha watanzania kufaidika na uanachama wa Tanzania katika Jumuiya mbalimbali za kikanda.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.Stergomena Tax wakati wa ufunguzi wa semina kuhusu “Nafasi ya Tanzania katika Mtangamano wa Kikanda” iliyotolewa na Wizara jijini Dodoma kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa lengo la kukuza uelewa kuhusu masuala ya mtangamano wa kikanda.

Dkt. Tax amesema kuwa, mtangamano wa kikanda ni dhana muhimu katika kukuza uchumi, kuimarisha uhusiano wa kisiasa, amani na usalama katika mataifa na kwamba Kamati hiyo ni miongoni mwa wadau muhimu wanaotakiwa kuwa na uelewa mkubwa kuhusu mtangamano wa kikanda ili kushirikiana na Wizara kueleza fursa na faida zake kwa wananchi.

Ameongeza kusema kwamba kwa Tanzania mtangamano wa kikanda ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje hivyo uelewa wa pamoja kuhusu dhana hii hususan fursa, faida na changamoto na namna ya kuzitatua unahitajika ili kufikia malengo kusudiwa.

Vilevile ameeleza kuwa, Tanzania inao mchango mkubwa katika Mtangamano wa kikanda na inategemewa ambapo pia imeendelea kunufaika na fursa mbalimbali zinazotokana na uanachama wake katika Jumuiya za Kikanda hususan, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ikiwemo ajira, biashara, teknolojia, elimu na uwekezaji.

Mhe. Dkt. Tax pia alitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa kila Jumuiya kwa kusisitiza kuwa kila Jumuiya ina umuhimu na mchango mkubwa kwa Tanzania kulingana na lengo la kuanzishwa kwake.

“Naomba niweke hoja hii sawa. Kumekuwa na ulinganifu wa utendaji wa Jumuiya hizi ambapo baadhi ya watu wanaona jumuiya moja ni bora kuliko nyingine pasipo kujua kwamba kila moja ina umuhimu wake kulingana na lengo la kuanzishwa,” amesema Dkt. Tax.

Akitoa mfano amesema SADC ilianzishwa kwa lengo la kupigania ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika. Hivyo kwa kiasi kikubwa Jumuiya hii imejikita kwenye masuala ya amani, ulinzi na usalama na kwamba ni kutokana na lengo hilo nchi za kusini zilikombolewa katika ukoloni lakini pia nchi wanachama kama Madagascar na Lesotho zilizokuwa na migogoro zimerejea katika hali ya amani na utulivu.

Kuhusu EAC amesema lengo la kuanzishwa kwake lilikuwa ni kuimarisha uchumi na biashara, hivyo kila jumuiya ni muhimu kulingana na majukumu yake.

Pia amesema anaishukuru kamati hiyo kwa kuendelea kushirikiana na Wizara kwenye masuala mbalimbali yenye maslahi kwa nchi na kuahidi kuendelea kushirikiana nayo katika masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje.

Akiwasilisha mada hiyo, Mkufunzi kutoka Chuo cha Diplomasia cha jijini Dar es Salaam, Bw. Charles Mtakwa amesema zipo faida nyingi kwa Tanzania kuwa mwanachama katika EAC na SADC ikiwemo ajira, biashara,elimu, teknolojia na uendelezaji miundombinu ya kikanda.

“Mtangamano wa Kikanda ni dhana muhimu kwa Tanzania na hususan
katika kukuza uchumi kupitia biashara, uwekezaji lakini pia kuboresha ufanisi wa soko la bidhaa mbalimbali kwani ni muhimu kwa nchi za Afrika kuendelea kukuza biashara miongoni mwake ambayo bado ipo katika kiwango cha chini cha asilimia 13 ukilinganisha na nchi za Bara la Asia asilimia 61 na Amerika asilimia 47” amesema.

Amesema kupitia Mtangangamano wa kikanda nchi wanachama huweza kufanya maamuzi ya pamoja ya kisera na kuchochea mageuzi ikiwemo yale ya kiuchumi. Pia kupitia mtangamano wa kikanda nchi wanachama hushirikiana kuchangia gharama za miradi mikubwa na miundombinu kama miradi ya umeme na miradi ya barabara na reli.

Ameeleza kuwa, Mtangamano wa Kikanda ambao unalenga katika kuziwezesha nchi wanachama kushirikiana katika masuala mbalimbali unazo hatua tano ambazo ni biashara huria;muungano wa forodha;soko la pamoja;muungano wa kifedha na muungano wa kisiasa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa amesema kuwa anaipongeza na kuishukuru Wizara kwa kuendelea kutoa semina kuhusu mada mbalimbali za umuhimu na kwamba Kamati hiyo itaendelea kutoa ushirikiano na ushauri unaohitajika kwa Wizara.

Kwa upande wao, Wajumbe wa Kamati hiyo wameishauri Wizara kushirikiana na wadau mbalimbali kuendelea kutangaza fursa zinazopatikana katika mtangamano wa kikanda na kuendelea kusimamia makubaliano na mikataba
iliyokwisha sainiwa katika kanda hizo ili itekelezwe kama ilivyopangwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akifungua semina kuhusu Nafasi ya Tanzania katika Mtangamano wa Kikanda iliyoandaliwa na Wizara kwa Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama 9NUU) iliyofanyika Dodoma hivi katibuni

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Vita Kawawa akizungumza wakati wa semina iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu Mtangamano wa Kikanda.