NA Mwandishi Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dk. Suleiman Serera, anaendelea na ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya elimu ya msingi inayotekelezwa wilayani humo na amesisitiza ijengwe kwa ubora, kuzingatia taratibu za ununuzi na kukamilishwa kwa wakati.
Katika ziara hiyo iliyoanza leo, Serera, ameongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED) ya Simanjiro, Samuel Gunzar, Kaimu Katibu Tawala, Mussa Waziri, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya na wataalamu kutoka idara za elimu ya msingi, ugavi na uhandisi.
Miradi hiyo inayokaguliwa inajumuisha iliyotokana na fedha za Serikali Kuu inayojulikana kama EP4R, BOOST pia iliyotokana na kuanzishwa kwa nguvu za wananchi na serikali.
Miradi hiyo ni ya ujenzi wa madarasa 40 mapya, ukamilishaji wa madarasa nane, nyumba sita za walimu (mbili kwa moja), ofisi, na matundu 55 ya vyoo. Gharama ya miradi hiyo ni Sh 1,633,150,000 na katika mchanganuo huo, Kijiji cha Namalulu kimepata Sh 638,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa shule kamili yenye miundombinu yote ikiwamo madarasa 16 (mikondo miwili), jengo la utawala, nyumba ya walimu na vyoo.
Ziara hii ya Serera na ujumbe wake pia inatarajia kutembelea na kukagua maeneo ya shule za Msingi Namalulu, Ormot, Naberera, Loiborsiret, Narakauo, Mbuko, Lemoot, Terrat, Oiborkishu na Komolo kisha itaendelea Mei 17, 2023 katika shule za Kandasikra, Endiamtu, Emishiye na Saniniu Laizer na kumalizia shule za Msitu wa Tembo, Majengo, Lemkuna, Ruvuremit, Loondrekes na Orkesumet.