Na Mwandishi Wetu

Tanzania, Burundi  na Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR)  zimesaini makubaliano ya pamoja kuhusu kuendelea kuwarejesha  kwa hiyari Nchini kwao Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa Nchini Tanzania makubaliano yaliyofikiwa mjini Gitega Burundi katika mkutano wa 23 wa pande tatu baina ya Serikali Jamhuri ya Tanzania, Serikali ya Burundi na Shirika la UNHCR.

Akizungumza katika mkutano huo  Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini akimuwakilisha Waziri mwenye dhamana amesema kuwa,  hadi kufikia tarehe 30 mwezi Aprili 2023 Tanzania  ina jumla ya Wakimbizi 175, 694 kutoka Burundi  ikijumuisha wakimbizi 49,234  walioingia tangu mwaka 1972.

Naibu Waziri Sagini amesema  tangu  kuanza kwa zoezi la kuwarejesha Wakimbizi mwezi Septemba 2017  mpaka sasa jumla ya Wakimbizi 146,204 wamerejea Burundi kwa hiari. Kutokana na kuwepo kwa idadi hiyo ndogo ya wanaorejea zoezi hilo bado limeendelea kuwa sio la kuridhisha  ili hali sababu kuu zilizowafanya kuja Tanzania wakiwa Wakimbizi kwa sasa haipo Nchini Burundi na ndio sababu iliyopelekea kuwepo kwa makubaliano hayo mapya.

“Tunatafuta suluhisho la kudumu la Wakimbizi waliopo Tanzania kurejea Nchini kwao. Wote tumekubaliana kama ambavyo Viongozi wetu wakuu walivyozungumza akiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan  na mgeni wake Mkuu wa Shirika la Wakimbizi Dunia haya ambayo tumeyathibitishwa katika makubaliano hayo.

Tanzania bado ni Nchi karimu lakini tulitaka kuona kunakuwa na uhiari wa Wakimbizi wa Burundi kurejea kwao kwa sababu ipo salama. Nami niwaombee Burundi muendelee kuwa na amani,muendelee kuwa na ushirikiano na mshikamano wa Taifa ili wanaporejea wawe na uhakika kuwa wanakwenda katika Nchi iliyosalama.”alisema Naibu Waziri  Sagini.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani, Usalama wa Raia na Maendeleo ya Jamii Jamhuri ya Burundi Mhe.Martin Niteretse amesema  mkutano huo umekuwa ni wa manufaa kwani Burundi imeendelea kuweka mipango ya kuwapokea na  kuhakikisha Wakimbizi hao wanarejea Nchini kwao.

“Tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwahifadhi ndugu zetu. Viongozi wa Burundi hatupendi kuendelea kusikia kuwa kunawatu wanaitwa Wakimbizi ilihali hali ya usalama na uchumi imeanza kuimarika.Uchumi wa Burundi unawategemea wao ili kwa pamoja tushirikiane kuijenga Burundi”Alisema Waziri

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kutoka Tanzania Mahoua Parums amesema shirika hilo litaishirikisha Jumuiya za Kimataifa kuweza kutoa fedha ili kuiwezesha Burundi kuwapokea Wakimbizi wake badala ya kuendelea kuwekeza nguvu katika ujenzi na upatikanaji wa huduma za kijamii katika kambi zilizopo Tanzania.

Parums ameongezea kuwa ili kuongeza idadi ya Wakimbizi kurejea kwao UNHCR itatoa kiasi cha dola 200 kwa  kila Mkimbizi atakayerejea Nchini Burundi badala ya dola 150 iliyokuwa ikitolewa awali ili kutoa motisha zaidi ya Wakimbizi hao kurejea kwa hiari Nchini kwao.

Serikali ya Tanzania inaendelea kushikamana na kuzingatia matakwa ya Kitaifa ikiwa ni pamoja na urejeshaji wa Wakimbizi katika Nchi zao kwa kuzingatia  makubaliano ambayo yameafikiwa