Hakuna ubishi kwamba baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa mkondo wa kwanza, hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika, uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga imejitengenezea ugumu mchezo wa marudiano.
Yanga inatarajiwa kukipiga na Al Ahly ya Misri huko Alexandrie mwishoni mwa wiki hii katika mchezo wa mkondo wa pili, na kushinda ni majaliwa kutokana na rekodi ya Wanajangwani pindi wanapokipiga na timu za Afrika ambazo wachezaji wake wana asili ya Uarab.
Ni mwaka juzi tu, ndipo Yanga kwa mara ya kwanza iliweza kuifunga Al Ahly ikiwa na kocha huyu huyo, Mholanzi Hans van der Pluijm ambaye jana alikubali sare ya 1-1.
Hata hivyo, katika mchezo wa marudiano Ahly walilipa kisasi kwa ushindi wa 1-0, hivyo mchezo ukahamia kwenye dakika za nyongeza na baadaye penalti, ambako ilitolewa kwa penalti 4-3.
Karibu miaka yote, Yanga inapocheza na Al Ahly inaonekana angalau inapata matokeo mazuri inapocheza Tanzania. Ikienda Misri inakumbana na majanga.
Tangu mwaka 1982, mchezo ujao utakuwa ni wa sita kwa Yanga kukipiga na Al Ahly kwani tayari zimekutana mara tano. Wa mara ya mwisho ni ule uliofanyika Jumamosi iliyopita.
Kabla ya mchezo wa Jumamosi iliyopita, mechi nne za zamani, Yanga ilitupwa nje Waarabu hao katika michezo yote lakini iliweka rekodi ya ushindi huo wa mwaka jana jijini Dar es Salaam.
Yanga ilishinda mchezo mmoja, kutoa sare mbili na kufungwa mchezo mmoja katika michezo minne iliyocheza Dar es Salaam dhidi ya timu hiyo, lakini ilifungwa michezo yote minne mingine ilipocheza ugenini nchini Misri.
Itakumbukwa kuwa mwaka 1982, Yanga na Al Ahly zilikutana katika hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga kulala kwa mabao 5-0 ugenini, lakini ikakomaa Dar es Salaam na kulazimisha sare ya bao 1-1. Hata hivyo ikafungashiwa virago kwa jumla ya mabao 6-1.
Zilikutana tena mwaka 1988 na katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka suluhu ya 0-0 na kisha Yanga kupigwa ugenini kwa mabao 4-0 na hivyo kutolewa raundi ya kwanza katika mashindano hayo.
Mwaka 2009, Yanga ilikubali kipigo cha nyumbani kwa bao 1-0 kutoka kwa Al Ahly pia ikafungwa ugenini mabao 3-0 katika mchezo wa raundi ya kwanza ya mashindano hayo na hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 4-0.
Lakini yote kwa yote, mpira unadumba hivyo inaweza ikawa bahati ya Yanga safari hii kufanya vema ugenini kwa kuwang’oa Waarab hao chini ya Pluijm baada ya kuvunja mwisho wa kutopata ushindi kabisa.
REKODI YA YANGA NA KASKAZINI AFRIKA:
1982: RAUNDI YA PILI: (Ligi ya Mabingwa)
Al- Ahly 5-0 Yanga SC (Cairo)
Yanga SC 1-1 Al- Ahly (Dar es Salaam)
1988: RAUNDI YA KWANZA: (Ligi ya Mabingwa)
Yanga SC 0-0 Al-Ahly (Dar es Salaam)
Al- Ahly 4-0 Yanga SC (Cairo)
2009: RAUNDI YA KWANZA: (Ligi ya Mabingwa)
Al Ahly 3-0 Yanga SC (Cairo)
Yanga 0-1 Al Ahly (Dar es Salaam)
2014: RAUNDI YA KWANZA: (Ligi ya Mabingwa)
Yanga 1-0 Al Ahly (Dar es Salaam)
Al Ahly 1-0 Yanga (Alexandrie)
(Yanga ilitolewa kwa penalti 4-3)