Lema akashinda. Lakini kutokana mwenendo wa kampeni ulivyokuwa, makada wa CCM ambao hawakuridhika, wakafungua kesi Mahakama Kuu na Lema akapigwa chini. Kama kawaida, wafuasi wa Chadema wakiwamo wana harakati na baadhi ya wasomi, wakamsuta Jaji aliyetoa hukumu hiyo kwa madai kuwa ilifanyika kisiasa.

Kwa maana nyingine, hukumu pekee ambayo ingezingatia haki ni ile tu ambayo ingemfanya Lema kuendelea kuwa mbunge! Inashangaza pia hata pale Dk. Makongoro Mahanga, Mbunge wa Segerea (CCM) alipombwaga Frederick Mpendazoe (Chadema), maneno yalikuwa hayo hayo.

 

Lakini, hukumu zilizowaondoa Khalfan Hayeshi wa Sumbawanga Mjini (CCM) na Dk. Dalali Kafumu (Igunga), baada ya Chadema kufungua kesi Mahakama Kuu, ndiyo zilikuwa halali na zilizozingatia haki! Haki kama hiyo ikitolewa kwa CCM, ni ya kisiasa na kuibeba CCM. Ndiyo tumefikia hapo.


Kabla hata matokeo ya urais hayajatangazwa, tayari Chadema wakaanza visingizio vilivyoashiria wazi maandalizi ya kuandaa vurugu nchini. Wakaanza kwa kudai kuwa kontena lililokuwa na karatasi za kupigia kura kuiwezesha CCM ishinde, wamelikamata Tunduma mkoani Mbeya. Kontena hilo baadaye lilidhihirika kuwa lilikuwa na shehena ya vipodozi!


Hili lilinikumbusha Profesa wa Uchumi Lipumba alipowahi kudai kuwa karatasi za kupigia kura za urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 zilichapishwa maalumu nchini China na kila mpiga kura akimchugua yeye, akiikunja alama inahamia kwa Kikwete!


Wakahamia kuituhumu Idara ya Usalama wa Taifa. Idara ikatuhumiwa kuwa inachakachua kura zake ili kumpa ushindi Dk. Kikwete!


Hivyo kama ilivyokuwa imetabiriwa na Watanzania wenye kuitakia mema nchi yetu, uongozi wote wa Chadema haukuhudhuria siku ya kutangazwa kwa matokeo pale katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam. Aidha, wakatangaza kutoyatambua matokeo ya Rais na hivyo hawamtambui Rais Kikwete. Kikawa ni chama cha kwanza tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 kumkataa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tena kwa staili mpya kabisa.


Wakijua wameingia bungeni kutafuta ulaji, wabunge wa Chadema wakaenda Dodoma kuapa. Wakashiriki kumchagua Spika na kupitisha jina la Waziri Mkuu lililopelekwa na Rais wasiyemtambua! Hapa ukanikumbusha umakini kabla ya kutenda jambo aliokuwa nao, Mabere Marando, Mbunge wa Rorya (NCCR-Mageuzi) wakati huo pale alipokataa kuapa pale Ukumbi wa Karimjee mwaka 1995 hadi kifungu fulani kiondolewe kwenye kiapo.


Lakini kwa udhaifu ule ule na uchanga wa siasa, Rais Kikwete alipolihutubia Bunge, bungeni Dodoma, wabunge wa Chadema wakatoka nje ya ukumbi, isipokuwa wachache ambao hata hivyo hawakuwapo ukumbini. Hawa nao wakapata misukosuko kutoka kwa wenye chama chao.


Kama kawaida, wanaharakati, wafuasi wao na baadhi ya wasomi wakawaona mashujaa! Kuanzia hapo, ikawa imepulizwa filimbi ya vurugu, hasa baada ya Katibu Mkuu wa Chadema kwa niaba ya chama chake alipotangaza kuwa “nchi haitatawalika”.


Viongozi wakaanza kuwahamsisha “makamanda wenye magwanda” kuingia popote kuvuruga au kuingiza wanayotaka katika mijadala na mikusanyiko ya masuala ya msingi ya jamii na nchi.


Wakaingia katika vyuo vya elimu ya juu, wakapanda mbegu chafu ya vijana waichukie Serikali, wakafadhili migomo na vurugu. Sote tunajua waliwatumia hata kuvuruga kazi ya kutoa maoni ya Sheria ya Kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

 

Tukashuhudia vurugu zilizofanywa na vijana walioandaliwa Dar es Salaam na Dodoma ambako ilibidi Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) kitumie mabomu ya kutoa machozi kuwatanya wanafunzi maeneo ya viwanja vya Bunge.


Wakaenda Arusha, katika viwanja vya Unga Limited, wakaandaa maandamano yaliyojaa vurugu ambayo vijana wa Chadema waliharibu vibaya Ofisi ya CCM ya Mkoa wa Arusha, kuvuruga biashara za wananchi na hatimaye vifo vya vijana watatu.


Siasa za maandamano ya kulazimisha ndiyo sera ya Chadema. Kila kiongozi ndani ya Chadema anaweza kutangaza maandamano na kuiamrisha Serikali. Hata Katibu wa Bavicha (Baraza la Vijana Chadema) wa Kata, anaweza “kumtaka Rais Kikwete”, “akampa siku saba IGP!”


Wakaenda Mbeya nako wakafanya maandamano na vurugu ambako kuliripotiwa kifo na majeruhi. Wakaenda Songea nako ni yale yale, yakatokea mauaji yaliyosababishwa na maandamano yao ya kuifanya nchi isitawalike. Wakaenda Morogoro, yale yale.


Septemba 2, mwaka huu kimetokea kifo cha kusikitisha cha mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi. Kifo kilichosababishwa na polisi, lakini chanzo kikiwa ni ubishi wa Chadema kukataa amri halali ya kuwataka kutofanya shughuli za siasa katika kipindi cha sensa.


Kifo cha Mwangosi kinasikitisha sana. Kinasikitisha kwa sababu akiwa mwanahabari ilibidi lazima aende katika tukio kupata habari. Tukio ambalo lisingetokea, bila shaka yasingetokea yaliyotokea. Kwamba, Chadema wangetii amri ya Polisi, kusingetokea yaliyotokea. Roho yake ilale mahali pema peponi. Amina.


Pamoja na matukio haya yote, viongozi wa Chadema badala ya kuyajutia matukio kama haya, yenyewe imeona kuwa ni mtaji mkubwa wa kisiasa na kwamba matukio kama hayo ndiyo yanawaongezea umaarufu na kukubalika kwa wananchi.


Kwao Chadema, kuanzisha vurugu na kisha watu kuuawa ni kafara ya kukubalika na umaarufu. Wanajua Watanzania hawataona kilichofichika, bali watakuwa wanajua Serikali ndiyo inawaonea. Wameaminishwa kukubali kuwa Chadema inaonewa na Serikali ya CCM. Wameaminishwa kukubali kuwa viongozi wa Chadema ni wasafi, waadilifu, wakweli na kila wanachosema ni sahihi na zaidi ni kwamba wana nia ya kuwakomboa.


Hawaamini kuwa Chadema na viongozi wake wamekuwa nyuma ya hujuma nyingi zinazofanyika nchini hivi sasa. Hujuma za kuchochea migomo, ingawa wamekuwa wakikanusha kwa madai kuwa wanachofanya ni kuwataka wanaogoma wasiache kudai haki zao na si kuwachochea!


Mtindo huu wanaoutumia Chadema una tofauti kubwa na siasa zilizokuwa zikiendeshwa na CUF hadi ikapachikwa majina yasiyofaa ya chama cha “Waislamu”, chama cha “Wapemba” n.k.


Staili yao ina tofauti kwani hata ndani ya Bunge, wabunge wao ni wapenda sifa ya kuonekana na kusikika wakisema tu, lakini si kwa kuisaidia Serikali na Watanzania. Kwangu mie, kama alivyowahi kusema mbunge mmoja, wengi wa wabunge wao ni kama wachekeshaji.


Lakini zaidi, mtindo wao wa kuzusha mambo tena ya hatari unaoungwa mkono na wanaharakati, baadhi ya wasomi na wafuasi wao unawafanya Watanzania wanaoitakia mema nchi yetu kuwatilia shaka.


Katika Tanzania watumishi wa umma wanaruhusiwa kuwa wanachama wa vyama vya siasa. Hivyo Chadema kama chama kina watumishi ambao ni wanachama wao, tena wale wa damu. Kwanini sisi tusiamini kuwa baadhi ya watumishi ambao ni wanachama wao ndiyo wanaoshiriki hujuma hizi? Kwa nini tusiamini kuwa, hata nyaraka za Serikali, nyingine za siri zinazokuwa mikononi mwa akina Dk. Slaa ni hao wanaozitoa?


Kwanini tusiamini kuwa vijana wa baadhi ya vyuo vya elimu ya juu wanachochewa na wahadhiri wao kugoma kama wapo wajumbe wa vikao vya juu kabisa vya Chadema ambao ni wahadhiri? Pia kwa nini tusiamini kuwa baadhi ya magazeti yanaandika uzushi iwapo yanamilikiwa na viongozi wa juu wa Chadema?


Hakika, kwa hali ilivyo sasa, na kama wataendelea, afadhali ya “ngangari” kuliko “magwanda haya ya makamanda wasio na mafunzo.”

Mungu ibariki Tanzania.

Mwandishi wa makala hii, Gabriel Athuman ni kada na mtumishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anayekitumikia chama hicho Makao Makuu Dodoma. Anapatikana kwa simu na. 0657861666. Haya aliyoyaandika hapa ni maoni yake, na kamwe hayahusiani na msimamo wa JAMHURI.