Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mkakati wa Serikali ni kumwezesha kila Mtanzania apate kitambulisho cha Taifa akiwa kijijini kwake.

Amesema hayo leo (Alhamisi, Mei 11, 2023) bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Mhandisi Ezra Chiwelesa kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Mbunge huyo alitaka kujua ni kwa nini Serikali haioni haja ya kuanza mchakato wa kuhuisha vitambulisho vya Taifa kama ilivyofanya kwenye zoezi la awali kwa kuwa kuna vijana wengi ambao wamefikisha umri wa miaka 18 na hawakupata fursa ya kujiandikisha kwenye awamu ya kwanza kwa hiyo hawana vitambulisho hivyo kama sera inavyotaka ikiwemo wananchi wa mikoa ya pembezoni.

Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na zoezi la utoaji wa vitambulisho kupitia taasisi ya NIDA ambayo awali ilikuwa na changamoto ya upungufu wa watumishi lakini hivi sasa imeshatatuliwa. “Awali tulikuwa na idadi ndogo sana ya watumishi wa kuweza kuwafikia wananchi. Kwa sasa tumeongeza idadi ya watumishi na ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuipongeza Serikali kwani vitambulisho vinatolewa kwa wingi.”

Waziri Mkuu amesema alishafanya ziara katika mikoa ya Kigoma, Kagera na Arusha (wilaya za Biharamulo na Longido) akakuta kuna changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho hivyo kwa sababu kasi ya utoaji ni ndogo. “Inawezekana kabisa wale ambao hawajafikiwa na hasa kwenye mikoa ya pembezoni, ni kutokana na kuwepo kwa changamoto ya muingiliano wa mataifa ya jirani. Kitambulisho hiki ni cha Taifa, na kinahusu usalama wa Taifa letu, tusingependa asiye raia awe nacho kwa sababu kitambulisho hiki ni mali ya Watanzania. Ndiyo maana, kwenye maeneo ya mpakani umakini unaongezeka.”

Waziri Mkuu amesema Serikali itawafikia wananchi zaidi kwa kuwapatia vitambulisho na wale ambao bado hawajapata, itawapatia namba za vitambulisho ili wazitumie kwenye mahitaji yao wakati wakisubiri kupatiwa[IK1]  vitambulisho hivyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inajipanga kupita kwenye maeneo yote yenye migogoro ili kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kulinda maeneo ya hifadhi.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini, Bw. Mwita Waitara ambaye alitaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kukomesha migogoro kwenye maeneo yaliyo jirani na hifadhi za Serikali.

Waziri Mkuu alilieleza Bunge kuwa Serikali ilishaanza kulifanyia kazi suala la mgororo wa Tarime kwa kuunda timu ya Mawaziri wa Ardhi, TAMISEMI na Maliasili na Utalii ambao aliwapa maelekezo ya kwenda kukutana na wananchi wa Tarime.

“Timu hiyo ya Mawaziri imefanya kazi na inakamilisha taarifa yao. Wataileta kwangu, tutaipitia na kisha tutakwenda kwa pamoja kuelimisha wanavijiji. “Sisi ndani ya Serikali tunaamini kuwa wananchi wanaoishi jirani na hifadhi ni walinzi wa kwanza wa hifadhi zetu.”

Amesema mkakati wa Serikali wa kukomesha migogoro hiyo ni kushirikisha wananchi wa maeneo yote ambako migogoro hiyo inatokea na kufanya mapitio ya pamoja ili kubaini mipaka inapita wapi. Amesema Serikali ilitoa maagizo kwa Mamlaka za Hifadhi ziweke vigingi virefu kwenye mipaka na vipakwe rangi nyeupe ili viweze kuonekana kwa mbali na kila mmoja aweze kuielewa kwa urahisi.

“Tunataka Watanzania tuone umuhimu kwa hifadhi na wahifadhi waone umuhimu wa raia wanaokaa pembezoni mwa hifadhi hizo. Tukiwa na dhana hii itatusaidia kutunza rasilmali zetu popote zilipo,” amesema