Benki ya NMB imekarabati na kukabidhi wodi ya uzazi pamoja na vifaa tiba kwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Ukarabati huo uliogharimu zaidi ya Shilingi Milioni 250 umejumuisha kupaka rangi jengo, kukarabati makabati, kubadilisha vyoo na kuboresha eneo la mapokezi. Pia umehusisha uwekaji masinki ya maji na miundombinu mingine.
Sambamba na ukarabati huo, Benki imekabidhi vifaa tiba ikiwemo vitanda vya kisasa vya kujifungulia, mashuka, mapazia, na vifaa vingine. Benki hiyo pia imeboresha eneo la mapokezi ya jengo hilo.
Katika kuhakikisha uangalizi wa wodi hiyo iliyopewa jina la ‘Jengo la Uzazi NMB’ unakua endelevu, Benki imesaini makubaliano ya miaka mitatu na uongozi wa hospitali, kuhakikisha ukarabati wa sehemu zilizobaki unaendelea kwa awamu.
Wodi hiyo imekabidhiwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB – Bi. Ruth Zaipuna kwa Waziri wa Afya – Mhe. Ummy Mwalimu mbele ya Mwenyekiti wa Bodi ya Muhimbili, Dkt. Ellen Senkoro; Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili – Prof. Mohammed Janabi na Mkuu wa Wilaya ya Ilala- Mhe. Edward Mpogolo na viongozi wengine wa Serikali, hospitali na benki katika hafla iliyofanyika hospitalini hapo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Ummy alisema Serikali inathamini mchango wa Sekta Binafsi katika kusaidia kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ya kitaifa, hivyo kuzitaka taasisi binafsi kuiga mfano wa NMB, aliyoitaja kuwa ni mshirika muhimu wa Serikali wa kuboresha afya za Watanzania, ambazo ndio mhimili mkuu wa ujenzi wa maendeleo ya taifa na uimarishaji uchumi.
“Kipekee kabisa niwapongeze NMB kwa ushirikiano endelevu baina yenu na Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye sekta ya afya. Kwa miaka yote 25 ya utoaji huduma kwa Watanzania, mmekuwa mstari wa mbele kusapoti ustawi wa maendeleo yao kwa kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, hivyo kusaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa Taifa letu kwa ujumla,” alisema.
“Tuko hapa leo kupokea wodi iliyokarabatiwa na benki yenu, ambayo pia inakabidhi msaada wa vifaa tiba, huu ni uthibitisho mnaotuonesha kwamba sekta binafsi inaweza kuchangia kuboresho huduma za afya nchini, ambayo ni haki ya msingi ya kila Mtanzania. Hiki mnachofanya hapa leo, kinaakisi namna benki yenu inavyojali ustawi wa wananchi, hususani kinamama na watoto wachanga,” alisema Waziri Ummy.
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna alisema: “Wazazi watakaojifungua katika Jengo la Uzazi la NMB, watapewa maarifa na elimu ya kuweka akiba kwa ajili ya watoto wao pindi watakapozaliwa. Pia wazazi wote watapewa kifurushi cha zawadi kutoka NMB chenye kadi ya pongezi, nguo maalum ya kupimia uzito wa mtoto atapopelekwa kliniki, kipima joto na zawadi nyinginezo.”
“Mwaka huu NMB inaadhimisha miaka 25 ya utoaji huduma tangu mwaka 1997, kwa kipindi chote hicho imekuwa mshirika wa karibu wa maendeleo. Kila mwaka tunatenga asilimia 1 ya faida yetu kurejesha kwa jamii kupitia Program ya Uwajibikaji (CSR), na kwa miaka 10 sasa tumetoa zaidi ya Sh. Bilioni 20 katika afya na elimu. Mwaka huu tumetenga Sh. Bilioni 6.2 ambazo ndani yake kuna fungu la kampeni endelevu ya upandaji miti milioni 1 ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,” alisema Zaipuna ambaye alibainisha kuwa kwa mwaka 2022 pekee, NMB ilitoa misaada mbalimbali katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zaidi ya 42 nchini, mchango uliosaidia zaidi ya Watanzania 210,000 kwa mwaka.
Naye Profesa Janabi, aliishukuru NMB kwa mkataba waushirikiano na uwekezaji iliyofanya katika Jengo la Uzazi Muhimbili, ambalo hutoa huduma za uzazi kwa zaidi ya wajawazito 210 kwa mwezi (sawa na wajawazito 70 kwa wiki na 10 kwa siku), wanaokimbizwa hapo toka hospitali mbalimbali na kwamba, benki hiyo imesaidia pakubwa katika kufanikisha kampeni ya kupunguza vifo vya kinamama na watoto kwenye hospitali hiyo inayojumuisha pia Tawi la Mloganzila – zote zikiwa na uwezo wa kulaza vitandani wagonjwa 2,300 kwa wakati mmoja.