………………………..

Watumishi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), 16 kutoka kada ya Mifumo ya kijiografia (GIS), Ulinzi, Usalama wa Anga, na Mawasiliano wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya ndege nyuki “Drone” pamoja na mifumo mbalimbali ya uendeshaji ndege zisizo na rubani ‘Drone’ yaliyofanyika Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara.

Mafunzo hayo ya siku 10 yaliendeshwa na kampuni ya Techno Enviroment Investment Co. ya Tanzania pamoja na kampuni ya ESRI East Africa ya nchini Kenya ambapo yalifunguliwa na Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara, Herman Batiho.

Matumizi ya ndege zisizo na rubani ‘Drone’ yapo ya aina mbalimbali, na kwa muda mrefu drone zimekuwa zikitumika kuchukua picha au video kutoka angani. Teknolojia hii ya ndege zisizo na rubani imekuwa msaada mkubwa sana kwenye majanga ya moto, pamoja na shughuli za ulinzi na usalama.

Vilevile drone zimekuwa zikitumiwa na wataalamu wa ardhi kuweza kupima na kutengeneza mipango bora ya matumizi ya ardhi.

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limekuwa likitumia teknolojia hii ya ndege zisizo na rubani “Drone” katika shughuli mbalimbali ikiwemo za ulinzi na usalama.