Uchaguzi Mkuu ujao hauko mbali kiasi cha kufanya Watanzania wachelewe kuanza maandalizi mapema. Ndiyo maana wengi hatushangai kuona na kusikia wanasiasa wanaojipanga sasa kwa ajili ya uchaguzi huo.
Baadhi ya watu wanatabiri kuwa uchaguzi huo utakuwa wa kihistoria kutokana na ushindani mkubwa wa vyama vya siasa unaozidi kushika kasi nchini. Hata hivyo, Watanzania tunapaswa kujihadhari tujise tukajikuta mwaka 2015 tunamkosa rais bora kutokana na vishawishi vya kinafiki na chuki binafsi.
Ninasema hivyo kwa sababu viashiria vya wanasiasa wanafiki, waliojenga chuki binafsi dhidi ya wengine na wenye uchu wa madaraka, vimeanza kuonekana katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu. Tanzania siku hizi imefika mahali ambapo baadhi ya wanasiasa wanaendelea kupata ujasiri wa kutaka kuwaaminisha watu kimakosa kuwa rangi nyeupe ni nyeusi!
Fikiria, kwa mfano, wanaosema hakuna maendeleo yoyoye yaliyopatikana nchini tangu tupate uhuru mwaka 1961. Huo ni unafiki wa dhahiri uliokuwa ajenda kuu ya baadhi ya wanasiasa. Mfumo wa vyama vingi vya siasa uliridhiwa nchini na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa lengo kuu la kuchochea mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, lakini yenye tija kwa Watanzania.
Kwa mantiki hiyo, vyama vya siasa havipo kwa ajili ya kupotosha na kufarakanisha wananchi, ili wanafiki na wenye uchu wa madaraka wapate mwanya wa kujineemesha na familia zao. Vyama vingi vya siasa vina faida nyingi, ambazo ni pamoja na kusaidia kukemea na kukosoa utendaji wa serikali iliyo madarakani inapoonekana kukiuka misingi ya uongozi bora ulio na manufaa kwa wananchi.
Lakini ukiona viongozi wa chama chochote cha siasa wanaelekeza nguvu kubwa katika kupanda mbegu ya chuki na kuwagawa wananchi, ujue hao ni wanasiasa ‘mcharuko’ wanaosukumwa na hisia za unafiki na kamwe hawaitakii mema nchi.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itajengwa na Watanzania wazalendo, wanaothamini umoja na mshikamano chini ya misingi ya amani na upendo – vilivyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, na Mzee Abeid Amani Karume.
Dhana za ubaguzi na utengano katika jamii zilipigwa vita kwa nguvu kubwa enzi za waasisi hao wa taifa letu. Mazingira hayo ndiyo sasa yanayowezesha hata viongozi wa vyama vya siasa kuzunguka na kuhutubia mikutano ya wananchi kila kona ya nchi bila kujali wanatoka wapi na wamezaliwa na nani.
Amani iliyojengeka nchini inaonekana kuwalewesha baadhi ya wanasiasa ambao pengine hawajui kuwa hata wao kama si familia, ndugu, jamaa na rafiki zao wanaweza kuathiriwa na machafuko ya kisiasa yanayoweza kutokea. Ongezeka la unafiki miongoni mwa wanasiasa linaweza kuwa sababu ya kumkosa kiongozi wa nchi anayetufaa ikiwa hatutakuwa makini katika kuchambua tabia za wanaowania madaraka hayo mwaka 2015.
Elimu ya siasa kama si ya uraia inahitajika kuwajengea Watanzania uwezo wa kutumia vizuri haki zao za kikatiba na kidemokrasia katika Uchaguzi Mkuu ujao; la sivyo watajikuta wamechagua rais ‘mtakavitu’. Serikali, vyama vya siasa na asasi za kiraia vina jukumu la kuwezesha elimu hiyo.
Suala hili ni muhimu katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu ili kuepuka hatari ya kumpata kiongozi wa nchi kutokana na ushawishi ulioasisiwa na hisia za unafiki, chuki binafsi na uchu wa madaraka.
Picha halisi ya kisiasa kwa sasa inaonesha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vinapewa nafasi kubwa ya kushinda kiti cha urais mwaka 2015, lakini hatuviweki kando vyama vingine vikiwamo Civil United Front (CUF), NCCR-Mageuzi na Alliance for Democratic Change (ADC). Yawezekana CCM na Chadema ndivyo vyenye ushawishi mkubwa kwa Watanzania, lakini pia vyenye ushindani mkubwa wa kisiasa nchini. Lakini tunachopaswa kuzingatia ni kutumia kigezo cha mtu badala ya chama kuchagua rais mwaka 2015.
Gharama za Uchaguzi Mkuu ujao ikiwezekana zielekezwe pia katika kuelimisha wajumbe wa vikao vyenye uamuzi ndani ya vyama vya siasa, kuhusu sifa za kiongozi bora kuwawezesha kufanya uamuzi sahihi katika uteuzi wa wagombea urais.
Zaidi ya hayo, Watanzania tujihadhari na wanasiasa wanafiki na wenye uchu wa madaraka, ili tusije tukajikuta katika Uchaguzi Mkuu ujao tunajinyima rais bora mwenye dhamira ya kuwatumikia wananchi kwa uzito unaostahili.