Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk.Albina Chuwa amesema Tanzania imeteuliwa kuingia kwenye kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa kuanzia mwakani kuungana na nchi nyingine 24 Duniani.
Dk.Chuwa ameeleza hayo jijini hapa leo Mei 3,2023 katika ufunguzi wa Mkutano wa Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na kusema mafanikio hayo yanatokana na utashi wa kisiasa wa serikali ya awamu ya sita katika masuala ya takwimu.
“Tanzania imeteuliwa kuingia katika kamisheni ya takwimu ya umoja wa mataifa kuanzia mwaka 2024 kwa kipindi cha miaka minne, hili linaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 24 Duniani zinazounda kamisheni hiyo. Mafanikio haya yanatokana na utashi wa kisiasa wa serikali ya awamu ya sita katika masuala ya takwimu,”.amesema
Amefafanua kuwa mpango huo unafadhiliwa na serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) na wadau wengine wa maendeleo ili kuboresha uzalishaji na usambazaji wa takwimu rasmi nchini.
“Katika utekelezaji wa mpango huu wadau kutoka serikalini na sekta binafsi watajengewa uwezo kupitia mafunzo ya muda mfupi na mrefu ikiwa ni pamoja na kujenga na kuimarisha mkiundombinu ya kitakwimu,”anaeleza
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Hamad Chande amewataka watumishi wa NBS kuwa waaminifu katika mchakato mzima wa uzalishaji wa Takwimu hasa wakati wa kuanzia kukusanya data, kuchakata data, kutafsiri data na utoaji wa taarifa.
“Tuwe wavumilivu kwa kuwa kazi za takwimu ni ngumu, zinahitaji muda na akili iliyotulia, hivyo tuvumilie kidogo tunachopata kwa maslahi mapana ya Taifa letu bila kulitia Taifa katika hasara,”anasisitiza.
Waziri huyo pia ametumia nafasi hiyo kuwataka watumishi wa NBS kuongeza ujuzi kila mara fursa inapopatikana ndani ya nchi na nje ya nchi, kwa kuwa nchi bado ina mahitaji makubwa sana ya kitakwimu hususan za hali ya umaskini wa watu ili kujua namna bora ya kuondoa umaskini katika ngazi zote za kijamii.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan inatambua mchango mkubwa wa wafanyakazi katika kuleta maendeleo ya nchi kutokana na nafasi yao katika uzalishaji wa bidhaa na utoaji huduma kwa jamii.
“Dhamira ya serikali ya Awamu ya Sita ni kuendelea kuboresha na kuimarisha ustawi wa Watumishi wote na kuwajengea mazingira bora ya kufanya kazi ili waweze kuzalisha na kutoa huduma bora zaidi kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe na maendeleo ya Taifa kwa ujumla;
Katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Awamu ya Sita tumeshuhudia hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya utumishi wa Umma. Miongoni mwa hatua hizo kama alivyoelezwa na Rais Dk.Samia wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka huu ambapo asilimia 93 ya madai ya wafanyakazi yaliyotolewa wakati wa Sikukuu ya Mei Mosi mwaka jana yametekelezwa,”amesema.