Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma.

Filamu ya Tanzania The Royal Tour imetimiza mwaka mmoja tangu ilipozinduliwa Aprili 28 mwaka jana Jijini Arusha huku ikielezwa kuleta matunda kwa Taifa ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya watalii na mapato kwa Serikali 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbas, amesema hayo leo Aprili 28,2023 wakat akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dodoma na kueleza kuwa sekta hiyo inaingiza asilimia 25 ya fedha zote za kigeni nchini.

Amesema kutokana na ongezeko la watalii nchini  filamu ya The Royal Tour imeongeza mapato ya sekta hiyo  kutoka sh. trilioni 3.01 mwaka 2021 hadi trilioni 5.82.

Aidha, watu zaidi ya bilioni 1.2 wameisikia, kuiona na kuifuatilia Tanzania kupitia filamu hiyo.

Dk. Abbas amesema watalii kutoka nje wameongezeka kutoka 620,867 mwaka 2020 hadi 1,454, 920 katika kipindi cha Desemba mwaka jana sawa na ongezeka la asilimia 57.7.

“Na kwa takwimu za mpaka Machi mwaka huu, inaonesha mwaka huu tutavunja rekodi ya Taifa kwa watalii kutoka nje.

“Watalii wa ndani wameongezeka kutoka 788,933 mwaka 2021 hadi 2,363,260 mwaka 2022,” ameeleza.

Katibu Mkuu huyo amesema  filamu hiyo pia imeleta manufaa kwa sekta ya usafiri wa anga ambapo miruko ya jumla ya ndege za kimataifa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) iliongezeka kwa asilimia 28 kutoka miruko 6,115 Aprili mwaka 2021 hadi 7,850 Aprili mwaka huu.

“Qatar Air na KLM waongeza miruko kwa siku kutoka tisa hadi 12 ikiwa ni ndege mbili kwa siku na miruko mitano hadi sita mtawalia kutokana na kuongezeka abiria baada ya Royal Tour.

“Ndege ya Eurowings Discover (Lufthansa Group) ilianza Juni mwaka jana kuja Tanzania mara mbili kwa wiki moja kwa moja kutoka Frankfurt, Ujerumani kuleta watalii wa Ujerumani na Ulaya kwa ujumla,” ameeleza.

Kwa upande wa uwekezaji Dk.Abbas amesema Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha Biashara nchini (TIC),  hamasa na mguso wa filamu ya Royal Tour imeongezeka.

“Akiwa Marekani mwaka jana, Rais Dk. Samia wakati wa Royal Tour alishuhudia mikataba nane ya awali ambayo miwili ikihusu sekta binafsi na sita ya kiserikali. Mikataba hii uwekezaji wake utafikia thamani ya zaidi ya sh. trilioni 11.7.

 “Baadhi ya wawekezaji hao wameshafika nchini na kupewa ardhi kama kampuni ya Camdemi HB (Hotel Arumeru), kampuni ya Polo Properties imeshasajili mradi TIC na kampuni za Northern New Feed zimeshafika nchini na taratibu zinaendelea.”

Please follow and like us:
Pin Share