Yanga-leo-72Katika historia ya soka, timu za Tanzania Yanga ikiwamo, hazina ubavu wa kuzitoa timu za Misri kwenye mashindano.

Lau Simba kidogo ambayo mwaka 2003, ilivunja rekodi kwa kuichapa Zamalek kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya wababe hao kulipa kisasi.

Lakini penalti ya mwisho ya kiungo Christopher Alex Massawe, ndiyo iliyowatoa Zamalek na kuvunja mwiko wa Waarabu kuzinyanyasa timu za Tanzania. Simba iliweza Yanga vipi?

Mtihani wa Yanga dhidi ya Wamisri unatarajiwa kuwa ama Jumamosi au Jumapili kadiri ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wenyeji Yanga watakaowakabirisha Al Ahly ya Misri.

Mchezo dhidi ya Al Ahly utakuwa ni mchezo wa kwanza wa Raundi ya Pili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambao wachambuzi wa soka wanasema utakuwa na ushindani wa aina yake.

Yanga na Al Ahly zitaanza kukutana mjini Cairo, Misri kwa mechi ya mkondo wa kwanza, na mechi ya marudiano itachezwa kati ya Aprili 19 na 20 jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Yanga kufikia hatua ya kucheza na Al Ahly iliwatoa APR ya Rwanda wakati wapinzani wao, mabingwa wa Misri, waliwatoa nje Klabu ya Recreativo Sesportivo do Libolo ya Angola ambao wametuma ujumbe Yanga wakisema wametolewa kwa bahati mbaya.

Yanga iliitoa APR kwa jumla ya mabao 3-2 kwa mechi mbili wakati Al Ahly iliifunga Libolo jumla ya mabao 2-0 baada kutoka Sare 0-0 huko Angola kushinda mabao 2-0 mjini Alexandria, Misri.

Kocha wa Libolo, Norberto Alves, anasema, “Yanga inaweza kuitoa Al Ahly. Nimeifuatilia Yanga kabla ya kucheza na Al Ahly nikijua ni wapinzani wetu wajao. Lakini kwa bahati mbaya walitutoa. Sasa ni zamu ya Yanga kuifunga Al Ahly.”

Ujumbe huo umepokewa vema na Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, akisema amemwelewa kocha mwenzake na kwamba amekipanga kikosi chake vema katika kuwafyeka Waarabu.

Kwa sasa anakiandaa vema kikosi chake na kwamba hadi kufikia mwishoni mwa wiki hii kitakiwa fiti kuisambaratisha Al Ahly. Itakumbukwa kwamba kwa mara ya mwisho Yanga ilikutana na Al Ahly katika michuano kama hiyo msimu wa 2013/14.

Yanga walishinda 1-0 mjini Dar es Salaam na Al Ahly kushinda 1-0 huko Misri na Al Ahly kusonga mbele baada ya kushinda kwa mikwaju ya penalti 5-3. Simba ilifanikiwa, safari hii ni zamu ya Yanga.

Pluijm, Mdachi anayeinoa Yanga kwa mafanikio akiwa na bahati na timu hiyo, amesema kuwa anaijua Al Ahly ni timu ngumu na inabidi wajipange ili waitupe nje na ndiyo maana wanajifua zaidi.

Lakini taarifa kutoka Misri zinasema kwamba Mkurugenzi wa Michezo wa Al Ahly, Syed Abdul Hafiz, amesema kwamba wanaifuatilia Yanga kwa karibu baada ya kuona inafanya vema kwenye Ligi Kuu Bara, aina ya wachezaji iliyonayo sambamba na kuitoa APR.

Amesema kwamba amesikitika hana baadhi ya taarifa za Yanga, lakini akajitutumua akisema wataiondoa Yanga kama walivyofanya msimu wa 2013/14.