Kwa mila na desturi za makuzi ya Kitanzania, tunafahamu uhusiano uliopo baina ya bibi na mjukuu. Kwa haraka tu, chochote akitakacho mjukuu kutoka kwa bibi, inakuwa rahisi kukipata.
Mahitaji ya mjukuu mara nyingi ni matunda na chakula, hivyo bibi akiwa na shamba lake inakuwa rahisi kwa mjukuu kwenda kuvuna ama matunda au chakula chochote akitakacho kutoka shambani.
Tena, mjukuu huchuma kwa madaha, akiamini kwamba hata kama hajaomba ruhusa kwa bibi, kwake ni ‘ruksa’ kuvuna akipendacho kutoka shambani–yote hii ni kwa sababu ni shamba la bibi.
Ndivyo ilivyogeuzwa Tanzania. Kila aliye na nafasi anachuma na kuburudika tu bila ya kufuata taratibu. Ndiyo maana Tanzania inaitwa ‘shamba la bibi’.
Hata Rais Dk. John Magufuli amethibitisha hili wiki mbili zilizopita, pale alipoamua kuchomekea maneno ya namna watu waliokasimiwa madaraka wanapofanya mambo ya ovyo ilhali wana akili, elimu na utaalamu.
Alichomokea maneno ya shamba la bibi alipokuwa akihutubia mamia ya wakazi Arusha huku akiwa amezungukwa na viongozi wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakati wa ufunguzi wa Barabara ya Sakina hadi Tengeru yenye urefu wa kilomita 14.1.
Barabara hiyo itakayokuwa ya njia nne itaunganisha Tanzania na Kenya.
Katika hotuba hiyo, Rais Dk. Magufuli anasema alikuta Serikali ikiwa na mambo ya ovyo.
“Tanzania hii, ilikuwa shamba la bibi, watu walikuwa wanafanya ya ovyo. Ninaposema ya ovyo ni ya ovyo kweli, mimi nipo serikalini, lakini nimekuwa waziri kwa miaka 20, ninayajua. Ninaposema ya ovyo, ndugu zangu naomba mniamini,” anasema Rais Dk. Magufuli.
Henry Batamuzi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kenwood Enterprises Tanzania yenye maskani Mbagala kwa Ngonyani, Mlandizi Kibaha mkoani Pwani.
Batamuzi anaishi huko Mlandizi, lakini angalau mara tano kati ya siku saba za wiki shughuli zake zinakuwa Dar es Salaam. Anatoka si chini ya kilomita 100, lakini kabla ya saa 12.00 asubuhi anakuwa jijini Dar es Salaam.
Sitaki kubeza, lakini ukweli ni kwamba wako baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam ambao wanaishi Ubungo, Kurasini, Mwenge, Magomeni na sehemu nyingi za jirani na ofisi zao ziko Posta, lakini hufika eneo la kazi jua limepanda.
Ole wako uhoji? Kisingizo kikubwa cha baadhi ya wafanyakazi ni foleni, mvua; askari wa barabarani nao wanabebeshwa lawama kwamba ama alisimamisha gari au foleni yao ilikuwa haivutwi. Mtanzania hakosi cha kujitetea.
Turudi kwenye mada ya msingi, katika kwapa la Batamuzi, hakosi mkoba. Humo pamoja na mambo mengine, anabeba nyaraka za uzalendo akipigania haki ya nchi. Mara kadhaa hufuatilia mambo ya ofisi yake, hasa biashara ya chuma chakavu ambayo kampuni hiyo ni mdau katika kununua na kuuza malighafi hiyo.
Hakuna ofisi ya Serikali ambayo Batamuzi hajaingia kuzungumzia biashara hiyo? Jibu la haraka bila shaka ni Ikulu ya Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, na zile za wasaidizi wake wa karibu kama vile Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na mawaziri.
Lakini baadhi ya ofisi ambazo Batamuzi amefika na kuzungumza na wakuu wa taasisi hizo kadhalika kuwaachia barua ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji; Usalama wa Taifa Mkoa wa Pwani na Makao Makuu; Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC); Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG); Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kwa Mwenyekiti Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Mbunge wa Kisarawe Seleman Jaffo, na kadhalika.
Huko kote anapeleka ‘jipu’ la biashara ya chuma chakavu. Lakini nani anajali? Wanampuuza tu, lau kwa wale wachache humjibu barua zake kwa kifupi tu: ‘Suala lako linafanyiwa kazi.’
Kampuni hiyo imefuata taratibu zote za kufanya biashara ya chuma chakavu, lakini cha ajabu ni kwamba haipewi nafasi ya kufanya biashara hiyo. Ina vibali kutoka NEMC vya kukusanya chuma chakavu, mabetri yaliyotumika na matairi yaliyotumika kutoka katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Vibali hivyo vinavyolipiwa kila mwaka jumla ya Sh milioni 1.3 ni kibali Na. NEMC/SM/2014/016 kinachohusu kukusanya chuma chakavu (Permit to collect Scrap Metals); Kibali Na. NEMC/WB/2014/004 cha kukusanya mabetri yaliyotumika (Permit to collect Used Lead Acid Batteries) na Kibali Na. NEMC/UT/2014/03 kukusanya matairi yaliyotumika (Permit to collect Used Tyres).
NEMC hutoa vibali hivyo kwa mujibu wa sheria (Issued Pursuant to Section 110 (1) of the Environmental Management Act Cap.191) na vibali hivyo vina masharti (Conditions of the Permit). Masharti ya NEMC ni kwamba kampuni haiwezi kufanya biashara bila ya kutimiza Sharti Na. 6 la mwongozo wa kununua na kuuza chuma chakavu.
Lakini Batamuzi anadai, “Kwa sababu ya uholela ulio katika biashara hii, wenye viwanda vya kuzalisha nondo wanaonunua chuma aina ya mild steel ikiwa ni malighafi ya viwanda vyao na wanunuzi wa chuma chakavu aina ya cast iron, copper, brass, aluminium soft na cast, stainless steel, used lead acid batteries na ambao wanasafirisha vyuma hivyo nje ya nchi (ingawa sheria inakataza), na kwa sababu ni uhalifu wa kupanga (organised crime).”
“Ni uhalifu wa kupanga unaofanywa na watumishi wa mamlaka zinazowajibika kusimamia biashara hii nchini kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, TRA (Customs), Idara ya Usalama wa Taifa na wamiliki wa viwanda vya kuzalisha nondo, madalali wao wanaofanya biashara ya mabilioni bila leseni ya biashara, TIN, VAT, usajili wa kampuni kutoka Brela, vibali kutoka NEMC au wengine wana vibali vya NEMC wakati hawana leseni ya biashara, TIN, usajili wa kampuni kutoka Brela!
“Biashara hii haifanyiki ipasavyo hivi sasa kutokana na uhalifu huu unaozuia kampuni zenye uhalali wa kufanya biashara hii. Hili ni jipu, labda baada ya kutumbua jipu hili kubwa ndiyo biashara hii itafanyika kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na wenye viwanda vya kuzalisha nondo kuingia mikataba na wafanyabiashara halali wa kuwauzia chuma chakavu na ndipo masharti ya vibali vinavyotolewa na NEMC yatatimizwa. Hii ni kazi ya NEMC.”
Batamuzi amefikisha malalamiko yake kule NEMC tangu Desemba 12, 2011 kuhusu biashara hiyo ikifanywa na baadhi ya wadau bila leseni (uhalali) hivyo kukwepa kodi, kuhodhiwa na wageni wanaoshindwa kuingiza fedha za kigeni, na kuwa chimbuko la hujuma kwa miundombinu ya reli, Tanesco, madaraja na kadhalika, lakini hadi leo imeshindwa kuyafanyia kazi.
Pia kuna hili la Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Kampuni ya Kuzalisha Mabati ya ALAF kuuza chuma chakavu kwa kampuni binafsi, lakini mambo huenda chini ya zulia.
Maeneo yaliyohujumiwa yameongezeka – Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Wakala wa Barabara Nchini (TanRoads), Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (Dawasco), Mkongo wa Taifa, viwanda vya nguo pamoja na uvuvi. Kuna meli ya uvuvi iliyokamatwa na Dk Magufuli wakati akiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambayo wafanyakazi wake walikuwa wakivua samaki bila ya kibali.
Batamuzi anasema, “Tunachotaka ni uwanja wa haki katika biashara hii. Tunataka sheria ifuatwe…biashara hii ifanyike kwa mujibu wa sheria na kila mamlaka serikalini isimamie sheria inayoihusu. Mamlaka husika zifungue uwanja wa mazungumzo kupitia Jumuiya za Wafanyabiashara ili upungufu na kasoro urekebishwe sekta binafsi iwe injini ya kuendesha uchumi wa Taifa hili. Mamlaka za kiserikali zifungue masikio na kuisikiliza sekta binafsi.”
Batamuzi aliwahi kumwandikia Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuomba kununua mitambo yote iliyokuwa Idara ya Upimaji na Ramani kwa barua yenye Kumb. Na. KWEDTL/SCRAPS/100/12 ya Februari 15, 2012 ikiwa na viambatanisho vya uhalali wa kufanya biashara pamoja na vibali vya NEMC kwa uthibitisho.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alijibu kwa barua yenye Kumb. Na. EA.251/450/01/134 ya Februari 27, 2012.
Naye Katibu mkuu alijibu: “Aidha utaratibu huo utakapokamilika utajulishwa ili uweze kushiriki katika zoezi la wazi la kununua vifaa hivyo.”
Batamuzi anasema, “ Inasikitisha na inauma sana kwa sababu nilikuta mitambo hiyo imeuzwa eti kwa wafanyakazi kama motisha! Je, walionunua mitambo hiyo chakavu waliinunua wakaifanyie nini? Je, ukifanya ukaguzi utaikuta bado ipo nchini? Huu ni uthibitisho kwamba raia wa mataifa mbalimbali wanaoishi nchini Tanzania na kufanya biashara mojawapo ya kuhamisha fedha zetu ni kununua chuma chakavu na kusafirisha katika nchi zao za asili.
“Hii inatokana na ububu wa kusababishiwa kwenye sheria mama ya fedha (Public Finance Act 2010 Disposal of Public Property; Regulation 257 of the Public Finance Regulations 2001), kwa sasa sheria hiyo haitofautishi (mauzo) ya mitambo chakavu (scraps) na mitambo kuu kuu (used) na inakaidi makusudi sifa za mnunuzi wa mitambo chakavu (scraps) na Sheria No. 21/2004 (Public Procurement of Goods, Works, Non-Consultant Services and Disposal of Public Assets by Tender),” anasema na kuongeza:
“Sheria hii kama haitatamka wazi namna ya kuuza mitambo chakavu, mapato ya Serikali yataendelea kupotea na watumishi wa Serikali wataendelea kujiuzia mitambo chakavu kama motisha wakati hawana sifa za kununua mitambo chakavu. Ni uhalifu ulioandaliwa (organized crime),” anasema.
Anatoa wito kwa Waziri wa Ardhi, William Lukuvi, akisema: “Nakuomba ofisi yako ifanye uchunguzi wa hujuma hii kwa uchumi wa Taifa na kama utapanua wigo wa uchunguzi kwa kampuni binafsi na taasisi za Serikali. Ukikagua mitambo ya yaliyokuwa mashirika ya umma tukayabinafsisha utakuta mitambo hiyo haipo.
“Vyuma chakavu vinavyozalishwa nchini kwa sasa vinauzwa kwa wenye viwanda vya kuzalisha nondo wakiwatumia madalali (nimejieleza kwenye barua yangu ya awali kwako), na chuma aina ya cast iron pamoja na non ferrous metal inanunuliwa na Wahindi, Wapakstan, Wachina, Warusi, Walebanon ambao hawana uhalali wa kufanya biashara hiyo na wanasafirisha kupeleka kwao. Ni biashara yenye athari kwa shilingi ya Tanzania, miundombinu ya reli, Tanesco, TTCL, Mkongo wa Taifa n.k., lakini kibaya zaidi inakuza deni la Taifa.”
Batamuzi anasema ili kudhibiti hujuma hiyo, anashauri hatua za haraka zichukuliwe na Serikali kama vile wenye viwanda vya kuzalisha nondo wanunue chuma chakavu (malighafi) kwa wenye leseni, na malipo yawe kwa hundi ili kuweka kumbukumbu na kukomesha ukwepaji kodi kubwa.
“Wanaosafirisha chuma chakavu nje ya nchi hawana leseni wala vibali vya NEMC vinavyowaruhusu kununua bidhaa hiyo na kusafirisha,” anasema Batamuzi na kuongeza:
“Duniani kote Tanzania tumekuwa nchi isiyosimamia sheria zilizotungwa na Bunge na kuendesha nchi kana kwamba hatuna Katiba. Raia wa kigeni wamenunua ardhi na kujenga viwanda vikubwa, vya kati na vidogo bila kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) lakini wanaitwa wawekezaji, hawalipi kodi.
“Na ni kinyume cha Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na; 4 na 5 ya mwaka 1999 lakini haisimamiwi, wanafanya watakavyo kana kwamba hatuna Serikali. Mifano ni mingi sana na inaaibisha, inatisha, Serikali inatulazimisha tuitwe Taifa masikini lakini wakati huo huo ni shamba la bibi kubwa duniani, Watanzania na wasiokuwa raia tunalazimishwa na Serikali tusilipe kodi katika biashara ya chuma chakavu,” anasema.
Anasema athari alizozitaja zisingekuwapo kama NEMC ingetumia mamlaka yake kisheria na kuandaa masharti ambayo pia kama yangesimamiwa vema Tanzania ingechuma fedha nyingi kutuepusha kuendelea kuwa ‘shamba la bibi’.
“Tatizo NEMC ni kuwa haina meno, imesogezwa mbali na Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo ni msimamizi wa biashara ya chuma chakavu nchini. Wizara hiyo iliunda Kamati ya Kanali Mayenga kukagua chuma chakavu inayosafirishwa nje bila kuitungia sheria,” anasisitiza.
Kwa hili, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk. Magufuli, haina budi kufahamu kwamba biashara ya chuma chakavu inafanyika bila leseni (uhalali), inakwepa kodi, inahujumu miundombinu ya reli, Tanesco, TTCL, Mkongo wa Taifa, TanRoads, Mamlaka za Maji Safi na Taka nchini, mashirika ya umma yaliyobinafsishwa, viwanda vya nguo na kadhalika.
Pia meli iliyokamatwa na Dk. Magufuli akiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambayo wafanyakazi wake walikuwa wakivua samaki bila ya kibali, nayo ilihujumiwa kabla ya kuzama. Kama Taifa, tunadaiwa Sh bilioni 3.3. Nani anabeba hasara hii?