Nilipokuwa mdogo, kuna wakati nilimsikia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akituhutubia. Naikumbuka hotuba yake yote, hebu tuikumbuke na wenzetu halafu tutafanya majumuisho tuone  je, inapaswa kuigwa?

Alisema: “Kila mwananchi anataka maendeleo; lakini si kila mwananchi anaelewa na kukubali masharti ya maendeleo.  Sharti moja kubwa ni JUHUDI.  Twendeni vijijini tuzungumze na wananchi kuona kama inawezekana au haiwezekani wananchi kuongeza juhudi.

Kwa mfano, katika miji, mfanyakazi wa mshahara hufanya kazi kwa saa saba na nusu au nane kutwa kwa muda wa siku sita au sita na nusu kwa juma.  Tuseme saa 45 kwa juma, kuondoa majuma mawili au matatu ya livu katika mwaka mzima.  Ndiyo kusema mfanyakazi wa mjini hufanya kazi ya saa 45 kwa juma kwa majuma 48 au 50 kwa mwaka.

Katika nchi kama yetu muda huu ni mdogo kwa kweli. Nchi nyingi hata zilizoendelea kutuzidi, hufanya kazi kwa muda mrefu zaidi kuliko saa 45 kwa juma. Si jambo la kawaida nchi changa kuanza na muda mfupi kama huo.  Jambo la kawaida ni kuanza na muda mrefu zaidi na kupunguza kila nchi inavyozidi kuendelea.  Sisi kwa kuanza na muda mfupi huu, na tunapodai muda mfupi zaidi, kwa kweli tunaiga nchi zilizoendelea. Na kuiga huku kunaweza kukatuletea majuto.  Lakini hata hivyo wafanyakazi wa mishahara hufanya kazi ya saa 45 kwa juma na livu yao kwa mwaka haizidi majuma manne. 

Yafaa kujiuliza wananchi wakulima, hasa wanaume, hufanya kazi kwa saa ngapi kwa juma na miezi mingapi kwa mwaka. Ni wengi mno ambao hawatimizi hata nusu ya wastani wa mfanyakazi wa mshahara.

Ukweli wenyewe ni kwamba vijijini kina mama hufanya sana kazi.  Pengine hutimiza saa 12 au 14 kutwa. Hawana Jumapili, na hawana livu.  Kinamama wa vijijini hufanya kazi kuliko mtu mwingine yeyote katika Tanzania. Lakini kina baba wa vijijini (na baadhi ya kina mama wa mijini) nusu ya maisha yao ni livu.  Nguvu hizi za mamilioni ya kina baba vijijini na maelfu ya kinamama wa mijini ambazo hivi sasa hazifanya kazi yoyote ila kupita soga, kucheza ngoma na kunywa pombe ni hazina kubwa na yenye manufaa zaidi kwa maendeleo ya nchi yetu kuliko hazina za mataifa matajiri.

Tutafanya jambo la faida kubwa kwa nchi yetu kama tukienda vijijini na kuwaambia wananchi kwamba wanayo hazina hii na kwamba ni wajibu wao kuitumia kwa faida yao wenyewe na faida ya Taifa letu.

Sharti la pili la maendeleo ni MAARIFA.  Juhudi bila maarifa haiwezi kutoa matunda bora kama juhudi na maarifa.  Kutumia jembe kubwa badala ya jemba dogo, kutumia jembe la kuvutwa na ng’ombe badala ya jembe la mkono; kutumia mbolea badala ya ardhi tupu; kunyunyizia dawa ili kuua wadudu; kujua ni zao gani lifaalo kupandwa na zao gani lisilofaa; kuchagua mbegu vizuri kabla ya kuzipanda; kujua wakati mzuri wa kupanda, wakati wa kupalilia n.k. ni maarifa yanayowezesha juhudi kutoa mazao mengi zaidi.

Fedha na wakati tunaotumia kuwapa wakulima maarifa haya ni fedha na wakati uletao faida kubwa zaidi kwa nchi yetu kuliko fedha na wakati mwingi tunaotumia katika mambo mengi tunayoyaita maendeleo.

Jambo hili kwa kweli tunalifahamu.  Katika mpango wetu wa miaka mitano mipango inayoendelea vizuri na hata kuzidi makisio ni ile inayotegemea juhudi ya wananchi wenyewe.  Pamba, kahawa, korosho, tumbaku, pareto, ni mazao yaliyoongezeka kwa haraka sana katika muda wa miaka mitatu iliyopita.  Lakini ni mazao ambayo yanaongezeka kwa sababu ya juhudi na uongozi wa wananchi, siyo kwa sababu ya fedha.

Kadhalika, wananchi kwa juhudi zao wenyewe na maelekezo au msaada kidogo wametimizi mipango mingi sana ya maendeleo huko vijijini.  wamejenga shule, dispensari, majumba ya  maendeleo, wamechimba visima, mifereji ya maji, mabwawa, mabarabara, wemejenga mabirika ya kukoshea mifugo na kujiletea wenyewe maendeleo ya aina mbalimbali.  Kama wangengoja fedha wasingeyapata maendeleo hayo.

Mipango inayotegemea fedha inakwenda vizuri lakini kuna mingi ambayo imesimama na yumkini mingine haitatimizwa kwa sababu ya upungufu wa fedha. Lakini kelele zetu bado ni kelele za fedha.  Juhudi yetu ya kutafuta fedha inazidi kuongezeka!  Siyo kwamba tuipunguze, bali, badala ya safari nyingi, ndefu na zenye gharama kubwa za kwenda katika miji mikuu ya mataifa ya kigeni kwenda kutafuta fedha za maendeleo yetu, itafaa kufunga safari kwenda vijijijni kuwafahamisha na kuwaongoza wananchi katika kujiletea maendeleo kwa juhudi yao wenyewe.  Ndiyo njia ya kweli ya kuleta maendeleo kwa kila mtu.

Hii maana yake si kwamba tangu sasa hatutajali fedha, wala hatutajenga viwanda au kufanya mipango yoyote ya maendeleo inayohitaji fedha… wala siyo kusema kuwa tangu sasa hatutapokea wala kutafuta fedha kutoka nchi za nje kwa ajili ya maendeleo yetu, LA, SIVYO.  Tutaendelea kutumia fedha; na mwaka hata mwaka tutatumia fedha nyingi zaidi kwa maendeleo yetu ya aina mbalimbali kuzidi mwaka uliopita,  kwani hiyo itakuwa ni dalili moja ya maendeleo yetu.

Lakini hii ni kusema kwamba tangu sasa tutajua nini ni shina na nini ni tunda la maendeleo yetu.  katika vitu viwili hivyo FEDHA na WATU ni dhahiri kwamba watu na JUHUDI yao ndiyo shina la maendeleo, fedha ni moja ya matunda ya juhudi hiyo. Tangu sasa tutasimama wima na kutembea kwa miguu yetu badala ya kupinduka na kuwa miguu juu vichwa chini. Viwanda vitakuja, na fedha zitakuja, lakini msingi wake ni WANANCHI na JUHUDI yao na hasa katika KILIMO.  Hii ndiyo maana ya kujitegemea.  Kwa hiyo basi, mkazo wetu na uwe: Ardhi na Kilimo, Wananchi, Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, na Uongozi bora.” Mwisho wa kukumbuka Mheshimiwa Rais.

 

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo.