Kamati iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan kutathimini utendaji kazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeanza kazi rasmi kwa kukutana na Waziri wa Wizara hiyo,Dkt. Stergomena Tax jijini Dodoma jana.
Wakati wa kikao hicho,Dkt.Tax aliwapongeza wajumbe wa kamati hiyo kwa kuaminiwa na Rais Samia na aliwaahidi kuwa Wizara itatoa ushirikiano unaohitajika ili Kamati hiyo iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
“Hii ni Kamati muhimu sana na ni matumaini ya Rais Samia kuwa mtafanya kazi nzuri itakayoleta mapendekezo yatakayoboresha utendaji wa Wizara ili kukidhi malengo ya Serikali ya kukuza diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa Kimataifa” alisema Dkt. Tax.
Dkt. Tax alisema wajumbe wa Kamati hiyo takribani wote ni wenyeji wa Wizara ya Mambo ya Nje na wabobevu katika masuala ya diplomasia, hivyo ana uhakika kwa muda waliopewa na hadidi za rejea walizopewa, watafanya kazi itakayokidhi matarajio ya Mhe. Rais Samia.
Kamati hiyo ina wajumbe 7 ambao ni mabalozi wastaafu; Hassan Simba Yahya, (Mwenyekiti), Ramadhani Muombwa Mwinyi (Mjumbe);Mwanaidi Sinare Maajar (Mjumbe); Peter Allan Kallaghe (Mjumbe); Tuvako Nathaniel Manongi (Mjumbe); Jack Mugendi Zoka (Mjumbe); na George Kahema Madafa (Mjumbe).
Kamati hiyo iliundwa na Rais Samia tarehe 28,mwaka huu.