Kama tujuavyo Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni chama kikongwe, ingawa ukongwe wake hauzidi ule wa Chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini kilichoanzishwa mnamo mwaka 1912. ANC ni chama cha siasa kikongwe zaidi barani Afrika.
Tanzania ni nchi ya vyama vingi. Lengo kuu la kuwa na vyama vingi hapana shaka ni kupanua demokrasia. Mfumo wa chama kimoja uliodumu Tanzania kwa miaka 27 kuanzia mwaka 1965 hadi 1992 ulibana demokrasia.
Katikati ya vyama vingi, ungetazamia CCM kuonesha mfano mzuri wa demokrasia inavyofanya kazi. Lakini mambo yamekuwa kinyume, CCM ndiyo inayoongoza kwa kubaka demokrasia nchini.
Tanzania inao utajiri mkubwa wa maliasili, lakini bado iko nyuma kimaendeleo, sababu moja kubwa ikiwa ni kwamba chama tawala na Serikali yake vimeshindwa kutumia vyema mfumo wa vyama vingi ambao ndiyo mfumo wa demokrasia na wa ushindani unaoleta maendeleo.
Nchi zilizopata maendeleo makubwa kama Uingereza na Marekani, ni nchi zilizotoa nafasi na uhuru mkubwa wa vyama vya upinzani kufanya kazi.
Nchi haiwi ya kidemokrasia kwa sababu tu ina vyama vingi, nchi inakuwa ya kidemokrasia vyama vyote vya siasa vinapopewa fursa sawa ya kufanya kazi zake.
Kwa upande wa Tanzania inaonekana kwamba bado CCM inaendeleza sheria ya mwaka 1975 ya chama kushika hatamu iliyoipa chama tawala madaraka ya kuongoza shughuli zote za umma.
Kwa hiyo, chama cha upinzani hakitakiwi kuongoza shughuli zozote za umma hata pale kinaposhinda uchaguzi. Ni katika mazingira hayo uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam umeendelea kukwamishwa na CCM katika kuhofiwa kwamba Kambi ya Upinzani itashinda uchaguzi huo.
Wakati CCM inaendelea kujigamba kwamba ni kinara wa mageuzi na kwamba iliruhusu mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kwa hiari yake, tuliokuwapo wakati huo tunajua ukuadi wa mambo.
CCM imezoea kutoa kauli zisizo na ukweli kana kwamba wakati yalipotokea mambo fulani walikuwapo wanachama wa CCM tu. Watu wengine hawakuwapo.
Kwa mfano, suala hili la Tanzania kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi. Baada ya vurugu za kisiasa zilizotokea nchi za Ulaya Mashariki kuanzia mwaka 1989 wakati wananchi wa nchi hizo walipokataa mfumo wa chama kimoja ulioendelea kuwakandamiza, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliona umuhimu wa kuepusha vurugu hizo Tanzania. Januari 1990 Kamati Kuu ya CCM iliruhusu mfumo wa vyama vingi. Kamati Kuu ilikataa kuruhusu mfumo wa vyama vingi, ilidai kuwa eti Watanzania hawahitaji vyama vingi, bali wanachohitaji ni maji na barabara nzuri.
Ndipo Mwalimu Nyerere akalazimika kuanzisha mjadala wa vyama Februari 1990 uliowataka Watanzania waamue kama walikuwa wanahitaji vyama vingi au waendelee kuwa na chama kimoja tu cha siasa.
Mwaka 1991 ikaundwa Tume ya Nyalali iliyokusanya maoni ya wananchi kuhusu mfumo wa kisiasa walioupendekeza. Tume ya Nyalali ilifanya kazi katika mazingira magumu yaliyosababishwa na CCM ambayo haikutaka Tanzania iwe na vyama vingi.
Kwa upande mmoja mikutano ambayo tume iliitumia kukusanya maoni ilitanguliwa na mchezo wa kuigiza ulioleta picha kwa Watanzania kwamba machafuko yaliyokuwa yakiendelea nchini Rwanda na Burundi wakati huo, yalitokana na nchi hizo kuwa na vyama vingi.
Lakini pia tume ilipangiwa kukutana na wanachama wa CCM tu, tena haikupewa nafasi ya kukutana na wasomi kama walimu na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Hivyo, asilimia 50 ya wanachama wa CCM waliokutana na tume walitaka Tanzania isiwe na vyama vingi, kiendelee kuwepo chama chao tu. Asilimia 20 ya wanachama hao wa CCM waliona hali mbaya ya mambo ya nchi iliyotokana na kukosekana kwa siasa za ushindani. Wakataka mabadiliko.
Kuanzia wakati huo, CCM imependelea kupotosha ukweli wa mambo kwa kudai kwamba asilimia 50 ya Watanzania hawakutaka vyama vingi wakati ni asilimia 80 ya wanachama wa CCM (na wala si Watanzania) waliokataa vyama vingi.
Hata Tume ya Nyalali ilipopendekeza Tanzania iwe na vyama vingi CCM iliendelea kupinga mpaka wafadhili walipohusisha misaada yao na mfumo wa vyama vingi. Kwa manufaa ya watoto wetu CCM isiendelee kupotosha historia ya kuingia kwa vyama vingi nchini.
Kwa kuwa Tanzania ilikuwa masikini, CCM ikabidi kukubali masharti ya wafadhili. Tukaingia kwenye mfumo wa vyama vingi. Lakini CCM haikupenda wapinzani wapate nafasi ya kuongoza jambo lolote nchini. Kwa hiyo, walitunga Katiba ya nchi iliyohakikisha kuwa Rais atatoka CCM wakati wote.
Wakazuia wapinzani kwenda mahakamani kuhoji matokeo ya uchaguzi wa rais, Tume ya Uchaguzi ikaendelea kutumiwa na chama tawala kuiba kura.
Katika uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, CCM inajua kuwa hakuna nafasi ya kuiba kura katikati ya kambi ya Ukawa yenye wapiga kura 87 na CCM yenye wapiga kura 76 tu. Ukawa wapewe haki yao, Dar es Salaam na Tanzania si mali ya CCM, ni mali yetu sote.
CCM ina wajibu wa kuzingatia mambo mawili. Kwanza, kwamba wajumbe wa Ukawa walichaguliwa na wananchi baada ya CCM kuboronga, hivyo basi hawakujichagua wenyewe, demokrasia inataka wengi wapewe. Pili, CCM izingatie pia kwamba bila haki hakuna amani. Amani inavunjika kwa sababu CCM inataka kukosesha haki wenye haki.
CCM iache kutuaminisha kwamba ni jipu lililoshindikana.