Wapenzi na mashabiki wa soka nchini wanasubiri kwa hamu kesho mtanange wa watani wa jadi – Wekundu wa Msimbazi, Simba Sports Club ya jijini na Dar es Salaam Young Africans (Yanga) yenye makao yake makuu mitaa ya Jangwani na Twiga, watakapopepetana kwenye Uwanja wa Taifa katika Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara.
Vijana wa Jangwani watatinga katika mtanange huo chini ya uongozi wa kocha wao mpya, Mholanzi Ernstus “Emie” Brandts, ambaye tayari ameahidi ushindi mnono wa timu hiyo dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi.
Brandts anayechukua nafasi ya kukinoa kikosi cha Yanga kutoka kwa kocha Mbelgiji Tom Saintfeit, aliyekifundisha kwa siku 77 na kunyakua Kombe la Kagame mwaka huu kabla ya kutimuliwa, ameahidi kukiwezesha kucheza kwa umahiri mkubwa na kung’ara msimu huu na kuua ndoto za Simba za kutwaa tena ubingwa.
Kwa upande wao, Simba, mabingwa watetezi wa Ligi hiyo, wameahidi kuendeleza kichapo katika mpambano huo wa kesho, ikiwa ni siku tatu baada ya kuinyuka Tanzania Prisons mabao 2-1, Jumamosi iliyopita.
Katika siku za karibuni, Simba imekuwa ikiwika mbele ya Yanga. Katika Ligi iliyopita, Simba ilijijengea heshima kubwa pale ilipoiadhibu Yanga bila huruma kwa kuishushia kipigo cha historia ya mara ya pili mabao 5-0 (baada ya ile ya mwaka 1977 ilipoiadhiri klabu hiyo hiyo kwa mabao 6-0).
Hata hivyo, Yanga imeahidi kurejesha heshima yake kwa kuhakikisha inaigaragaza Simba mbele ya mashabiki wa soka katika kila mechi watakayokutana, ikiwamo hiyo ya kesho. Dodoso za hapa na pale zinasema kila timu imejipanga kuhakikisha inacheza kwa tahadhari kubwa kuepuka zahama za kufungwa, majeruhi na kadi nyekundi.
Majeruhi na kadi nyekundi ni miongoni mwa vitu hatari vinavyochangia kupunguza nguvu ya timu za soka katika mashindano. Mashabiki na wapenzi wa timu hizo wanatarajiwa kuhudhuria kwa wingi kushuhudia moja kwa moja mpambano huo katika Uwanja wa Taifa, huku kila upande ukitarajia kuona timu yake inaibuka na ushindi.
Ni dhahiri kuwa mchuano huo utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na kila timu kuahidi kutowakosesha raha mashabiki wake, kwa kuhakikisha inaondoka dimbani kifua mbele kwa kuibuka na ushindi wa kihistoria. Matokeo ya mechi hiyo ya kesho ndiyo yatakayowadhihirishia wapenzi na mashabiki wa soka ukweli wa tambo za kila timu.
Siku zote watani hao wa jadi wamekuwa wakitambiana kuoneshana ubabe, lakini tumekuwa tukishuhudia upande mmoja ukiondoka uwanjani vichwa chini, mikono kichwani na kiunoni baada ya kutandikwa bila huruma. Matarajio ya wengi ni kwamba kwa kesho, si Simba wala Yanga itakayohakikisha inaweka rekodi nzuri kuondoka uwanjani na ushindi mnono.
Ujio wa kocha mpya wa Yanga, Mholanzi Brandts, bila shaka umefanya kocha wa Simba, Milovan Cirkovick, kubuni mbinu nzuri zaidi za kukinoa kikosi chake ili kuonesha makali yake kwa Brandts. Lakini Brandts naye bila shaka amejipanga kuhakikisha katika mechi hiyo ya kwanza chini ya uongozi wake, wana-Jangwani wanawaaibisha Wekundi wa Msimbazi.
Wachezaji wa timu zote wamenolewa vilivyo kuhakikisha wanacheza kwa umahiri mkubwa utakaowezesha kupata ushindi, lakini pia kukonga nyozo za wapenzi na mashabiki wao.
Ni ukweli usiopingika kuwa bado timu zote hizo zina nafasi ya kufanya vizuri katika mpambano huo, kutokana na kila timu kusheheni wachezaji wengi wazuri na wenye vipaji.
Lakini Simba wameendelea kuonesha ubabe katika soka, hata baada ya mchezaji wake mahiri, Emmanuel Okwi, kutolewa kwa kadi nyekundu na kumfanya kutumikia adhabu ya kukosa michezo mitatu. Simba iliweza kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Ruvu siku hiyo.
Katika mechi iliyochezwa kwenye dimba la Taifa Jumamosi iliyopita, Simba bila ya Okwi ilitupia Tanzania Prisons mabao 2-1, ikionesha kuwa lolote linawezekana.
Simba bado inang’ang’ania kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwa kuwa na point 12 kibindoni.