Mzanzibari mwingine yeye katamka maoni yake hivi, “…endapo chama hicho cha CUF kitasusia uchaguzi huo, kitapata hasara za namna mbili. Mosi, kupoteza madaraka kwa viongozi wake wa juu na pia kuondoa ushawishi wa chama hicho kwenye maamuzi muhimu ya Zanzibar kwa kipindi kirefu cha miaka mitano ijayo. (Hamad Rashid Mohamed katika Raia Mwema toleo No. 442 la Januari 27– 2 Februari, 2016 uk. 3).
Mzanzibari mwingine ameandika kwa kirefu makala: “Naziona Unguja, Pemba zikigawanyika” hapa nakunakilia haya machache. Amesema hivi, “Ninathubutu kuandika makala haya ili kuweka vyema kumbukumbu na iwapo Mungu atanichukua, basi ikumbukwe kuwa nimewahi kusema kuwa ninaota na kuona Visiwa hivi kuwa haviwezi kuendelea kuwa pamoja na kubaki salama.
Kadiri ninavyoyapekua matukio ya kihistoria ya Zanzibar kabla ya ujio wa wakoloni na baadaye Waafrika kujitawala, ninayaona makundi mawili hasimu na yasiyosikilizana miaka nenda rudi yakiwa yanavutana na kukwaruzana; watu wa Unguja na Pemba.
Kilichoonekana zaidi wakati wote huo ni idadi kubwa ya Wapemba kuanza kuhamia kwa nguvu Unguja na kuweka makazi ya kudumu na Waunguja wakiwa hawapati hamu ya kuishi Pemba.
Wapemba na Waunguja hadi sasa wamebaki kuwa marafiki wa mashaka. Hawaaminiani, wala hawawezi kusafiri masafa marefu wakiwa wamoja bila katikati ya safari yao kubaguana kila wapeanapo visogo.
Idadi kubwa ya watu kutoka Pemba tangu enzi za ukoloni hawakuiunga mkono ASP kuelekea Uhuru, hawakushiriki Mapinduzi ya mwaka 1964 na wala hawakuunga mkono wazo la Zanzibar kuungana na Tanganyika.
Mtu mwenye maarifa, msema kweli na asiyeficha mambo atashindwaje kusema kuwa Pemba inalazimishwa kibabe kutii mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wapemba wanakubali kwa shingo upande tu” (Mwandishi wetu Zanzibar katika Raia Tanzania Toleo No. 0532 la Jumatatu Desemba 21, 2015 uk. 21) tafadhali kajisomee makala yote ile.
Hapo wasomaji mmeweza kupata picha kutoka kwa Wazanzibari wenyewe na mkatafakari kwa nini tatizo lote la kule Visiwani halimalizwi. Upo mvutano wa asili kati ya Wapemba na Waunguja.
Pili, ni vigumu kumtambua nani kule Visiwani ni mzalendo wa kweli na nani ni kibaraka wa lile kundi la mabwenyenye waliokimbia baada ya Mapinduzi hali wangali na usongo wa mali zao zilizotaifishwa wakati wa Mapinduzi.
Tatu, mtakumbuka enzi zile za utawala wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Sheikh Abeid Amani Karume, alipata kusema,“Wageni hapa Visiwani wameoana na dada zetu na mabinti zetu sasa ni ruksa kwenu Waafrika wa Visiwani mkitaka oeni Waarabu, Wahindi na Wazungu”. Matamshi yale yaliwatia ukakasi sana Waarabu na Wahindi na ndipo wakakimbiza mabinti zao kwenda nje ya Zanzibar.
Tamko lile Waarabu waliona wamedhalilishwa. Kuna wakati hata Tume kutoka Amnesty International walitumwa Visiwani eti kuchunguza MBM wangapi wameoa Waarabu kwa ndoa za kulazimishwa.
Haya yote ya eti nyinyi mlikuwa Hizbu au ASP ni geresha za kisiasa tu. Kuna hofu na wasiwasi kutoka pande zote mbili za vyama vile vikuu kule Visiwani. Chama kimoja kimekuwa na sera ya kuwakaribisha wale wote waliokimbia baada ya Mapinduzi kule Visiwani kwa ahadi ya kuwarejeshea ardhi yao ya awali eti iliporwa na Wanamapinduzi. Huku chama kingine kwa upande mwingine (chama tawala) wanasema hawapo tayari kabisa kuona ubepari wa mabwenyenye wa Kiarabu unarudi Zanzibar.
Isitoshe, kutokana na upungufu mkubwa wa makazi huko Visiwani, jarida moja liliandika hivi “given the shortage of housing in Zanzibar it is unlikely that the pattern of multi-family occupancy could be reserved!” kweli kule Stone Town mwananchi mkazi wa leo ahame na kumpisha Mwarabu au waishi nyumba moja, ni jambo lisilofikirika wala kukubalika. Hapo sasa ndipo utata wa siasa za Visiwani ulipolala.
Kwa mara nyingine tena ndipo tunakumbushwa na Balozi Amina kwa wazi anaposema namnukuu “kuwa mijadala ya mwafaka imefanyika mara 9 kati ya viongozi wa CCM na wa CUF. Wameshakutana lakini hawajaweza kufikia mwafaka”. Ugumu wa kufikia uamuzi mzito ndipo Mngoni anasema “iyi hinu ndindani” – ushindani usiomalizika.
Hebu kimawazo niwarudishe tena nyuma kidogo (rewind your memories) wasomaji wangu wapenzi imekuwaje suala hili la Wapemba na Waunguja kutokumalizika kidugu na kiupendo (amicably and brotherly). Nimesoma katika kijarida kimoja kiitwacho Radi.
Mle nimesoma swali hili, “Kwanini Wakili ameondoka? Katika kijarida kile kumetolewa mlolongo wa sababu. Imeandikwa hivi, “tangu kabla ya uchaguzi ule wa mwaka 1985 kumekuwa na matukio mbalimbali yaliyokinzana kimawazo miongoni mwa viongozi wa Zanzibar. Kuingia kwa Wakil kwenye madaraka kumrithi urais wa SMZ Mzee Mwinyi aliyechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kulikuwa kama kumshikisha huyo Mzee Wakili uongozi wa mtumbwi katika ziwa au bahari iliyochafuka kwa mawimbi makali. Basi uhodari wake nahodha ilibidi uonekane katika hatua za mwanzo za kuokoa chombo na waliomo. Ilitakiwa aungwe mkono na apate ushirikiano wa dhati toka kwa Wazanzibari wote” (tazama Radi Toleo la Septemba 8, 1990 uk 18).
Bahati mbaya haikuwa hivyo. Nini basi kilitokea katika azma hiyo muhimu katika unahodha wa huko Visiwani? (Urais) Radi imetoa matokeo ya kura zilizopigwa wakati wa Uchaguzi ule wa 1985. Ninukuu matokeo yenyewe hapa mjisomee matokeo kati ya Waunguja na Wapemba.
Kutoka Unguja Wakil alipata kura 109,593 za ‘ndiyo’; kura 11,208 za ‘hapana’ wakati kura zilizoharibika zilikuwa 3,463. Wapiga kura 8,653 hawakujitokeza kutumia ile haki yao ya kuchagua kiongozi wanayemtaka. Hapo Unguja waliojiandikisha kupiga kura walikuwa jumla ya wananchi 124,264.Kwa matokeo hayo Mzee Wakil alikubalika kwa 88.19% na wananchi wa kisiwa cha Unguja.
Je, kule Pemba nako wananchi walimpokeaje? Kule Wakil alipata matokeo namna hii:- Kura za ‘ndiyo’ alipata 21,880, kura za ‘hapana’ alipata 64,004. Kura zilizoharibika zilikuwa 3,575 na wasiotumia haki yao ile ya kuchagua Rais au Kiongozi wanayemtaka walikuwa 8,386. Hapo inaonekana Wapemba waliomkubali Wakili kuwa Rais wao walifikia 24.46% tu. Kumbe Wapemba wengi basi walimkataa! Jumla ya Wapemba wote waliojiandikisha kwa upigaji kura katika daftari la wapiga kura walifikia idadi ya watu 97,842.
Kwa matokeo namna hii Mzee wetu Wakili aliona alivyokataliwa kule Pemba. Hili lilitosha kumkatisha tamaa ya kuongoza lile jahazi la SMZ kwa uhakika na kwa ridhaa ya Wazanzibari wote.
>>ITAENDELEA