Siku moja watoto watundu walikuwa wakicheza kwenye uwanja, karibu na bwawa. Wakacheza mpira, wakacheza mchezo wa kukimbizana na michezo mingine mingi. Mwisho walichoka na michezo yao wakaenda kwenye bwawa.

Waliokota mawe na kuanza kuyatupa ndani ya bwawa walimokuwa vyura. Kila walipoona chura amejitokeza walitupa mawe. Waliendelea na mchezo huo kwa muda mrefu.

Mwisho chura mmoja mzee alijitokeza nje ya maji na kusema, “Enyi  watoto. Inaonekana hamwelewi kuwa mambo mnayoyafanya ingawaje ni mchezo kwenu, lakini ni mauti kwetu.”

Nimenukuu hadithi hiyo, WATOTO NA VYURA  kutoka kitabu  Hadithi za ESOPO, kitabu cha kwanza. Nilikisoma miaka 58 iliyopita nilipokuwa mtoto wa shule ya msingi. Lengo la kunukuu ni kutaka kufananisha michezo iliyofanywa na watoto wale na kauli zinazotolewa leo na baadhi ya viongozi wetu wa siasa na Serikali.

Natambua wapo baadhi ya wanachama wa vyama vya siasa na raia wa serikali hawapendi na hawataki viongozi wao kusemwa hata kama wanataja maneno yenye dalili ya kuleta utengano, uvunjifu wa utulivu na kusimika uhasama ndani ya jamii yetu iliyotangamana. Kwa hili, nawataka radhi kwa hayo nitakayoyasema.

Ni busara watu kama hao wazuie hasira na mihemuko yao na wakae tuli na kutafakari kauli za viongozi wao zitolewazo zinajenga utulivu au zinastawisha chuki na kulisukuma taifa kwenye mapigano au vita vya wenyewe kwa wenyewe?

Uungwana unatutambulisha na kutuelimisha kuwa daima katika kinyang’anyiro chochote iwe cha michezo, siasa, mapenzi na kadhalika matokeo ya kupata au kukosa hayana budi kutokea kwa mshindani mmoja wapo. Ndiyo maana wahenga wametwambia: “Asiyekubali kushindwa si mshindani.”

Wamekwenda mbali zaidi na kusema: “Penye udhia penyeza rupia” kwa maana kuondoa udhia huo washindanao wakae kwenye meza ya duara ya mazungumzo na kujadili mwenedo mzima wa mashindano na mwishowe kutoa uamuzi jadidi. Sio tena kuanzisha malumbano mapya.

Si hayo tu. Wahenga na watu makini waliojaa hekima na busara wanatambua kukaa kimya si ujinga wala kuogopa bali ni kutafakari sababu na mbinu zilizosababisha kushindwa. Tafakuri hiyo hutoa majibu maridhawa na kutibu donda la kushindwa.

Ningependa kusema mengi, lakini nachelea muda. Nasema masikio ya watu yanapokea milio lufufu ya kauli za viongozi mbalimbali zenye kutia hofu, mashaka na wasiwasi mioyoni. Dalili za kupoteza furaha upendo na amani zinaonekana kutokana na milio ya wanasiasa dhidi ya serikali.

Kasi ya Serikali ya utumbuaji wajipu na kauli zake zinawatisha wanasiasa wapinzani, huenda na wao wakatumbuliwa! Vibano vya udiwani, umeya na kauli za wapinzani ni vitasa kwa serikali ambayo sasa inapumua kwa shida katika baadhi ya Halmashauri na Manispaa zake kutokana na usaliti ulifanywa na watendaji wasio waadilifu.

Yanayotokea Zanzibar katika mizani ya kauli na vitendo vya Serikali, CUF na ZEC zinapanua wasiwasi kwa wananchi. Ni uungwana na ustaarabu kwa vyombo nilivyovitaja kurejea katika mazungumzo ya kutafuta mwafaka au upande mmoja kusema haidhuru; mambo yameisha tugange yajayo.

Kusema haidhuru si ujinga, ubwege wala woga bali ni ustaarabu uungwana na ushujaa wa ujasiri. Kumbuka watoto watundu wale waliposikia maneno ya chura mzee waliacha kutupa mawe bwawani na ukawa ndiyo usalama wa vyura wale.

Chura mzee alitumia hekima na ujasiri kuwaeleza watoto. Nao watoto waliheshimu kauli yake na kutambua thamani ya uhai si kwa binadamu tu bali hata kwa wadudu, ndege, wanyama na viumbe vilivyomo majini; lau kama walikuwa na uwezo na mawe ya kuwatupia na kuangamiza uhai wa vyura wale.

Lipi ni tatizo ambalo vyama vya siasa; CCM, CHADEMA, CUF, Serikali na ZEC na wengineo kukaa pomoja kilingeni kunusuru amani  yetu isitoweke na badala yake kila mmoja wenu kutoa kauli za vitisho na kuandaa ubabe dhidi ya mweziwe. Hivi kati yenu nani ni mbabe zaidi ya Mwenyezi Mungu?.

Wala msitie akilini eti mkifanya ubabe na ung’ang’anizi wa kauli zetu mnatufurahisha, hapana. Hapana hata kidogo kwa watu tulio na akili timamu. Mnatutia mashaka na kimuhemuhe moyoni. Hamkuumbwa kutaka kutawala na kuua. Mmeumbwa kuishi na kuijaza dunia. Dunia ni watu si malumbano. Malumbano ni uwanja vifo.

Hivi kati yenu yupi ana uhakika wa kuishi kesho hadi mtondo? Anasa za kutaka sifa kutawala isicheleze na upondo utakaokurusha hadi kwenye zama za utawala ili hali chini ya upondo kuna mauti.

Chura mzee na watoto watundu walielewana lau kama wanatofautiana maumbile, rika na mazingira ya kuishi. Aibu iliyoje ninyi ni viumbe wa aina moja, rika za kufanana na mazingira moja ya kuishi. Kulikoni?