Joyce NdalichakoMatokeo ya mtihani wa kidato cha nne yametangazwa siku nyingi kidogo na watu wengi wamejitahidi kuyachambua. Kwa kuwa na mimi ni mdau wa elimu nachukua nafasi hii kuyachambua.

Kuna mambo makubwa yaliyojitokeza katika matokeo ya mtihani huo. Kwanza, kuendelea kufanya vibaya kwa shule za Serikali katika mtihani huo. Pili,  kutumika kwa mfumo wa madaraja (divisheni) katika upangaji wa matokeo badala ya mfumo wa wastani wa alama (GPA). 

Kutumika kwa mfumo wa madaraja kumetusaidia sana kujua hali halisi ya mambo. Shukrani za dhati kwa Waziri wa Elimu, Dk. Joyce Ndalichako, aliyehakikisha kutumika mfumo huo wa madaraja. 

Tatu, kuandikwa kwa historia ya shule ya Sekondari ya Kaizirege iliyopo mkoani Kagera iliyofaulisha watahiniwa wote 72 kwa ufaulu wa daraja la kwanza.

Nne, kitendo cha mwanafunzi raia wa China, Concong Wang, wa Shule ya Wasichana ya Feza mkoani Dar es Salaam kwa kushika nafasi ya pili kitaifa katika mtihani huo. 

Congcong Wang alipata alama B katika Kiswahili na kuwapiga kumbo maelfu ya wanafunzi Waswahili wa Kitanzania waliofeli somo hilo. Lakini pia mwanafunzi huyo alipata alama A katika somo la Civics (Uraia) na kuwapiga kumbo tena wanafunzi wa Kitanzania waliotazamiwa kujua zaidi masuala ya uraia wa Tanzania.

Shukrani kwa Butogwa Charles Shija wa Shule ya Sekondari ya Cannosa, Dar es Salaam, aliyeshika nafasi ya kwanza katika mtihani huo kitaifa. Amelitoa aibu Taifa la Tanzania vinginevyo yule raia wa China angeshika nafasi ya kwanza.

Wakati huo huo, matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yameonesha kuwa kiwango cha ufaulu wa somo la Kiswahili ni wa juu sana wakati ufaulu katika somo la Hisabati ni wa chini kabisa.

Kiwango cha ufaulu wa somo la Hisabati ni wa chini pia hata katika mtihani wa darasa la saba shule za msingi. Kwa kweli kuna haja ya kuitishwa kongamano ambalo litatafuta sababu ya somo la Hisabati kuendelea kufanywa vibaya wakati wote.

Sasa tuchambue sababu zilizotajwa za shule za watu binafsi kufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne na sababu za shule za Serikali kufanya vibaya.

 Sababu zilizotajwa na wamiliki wa sule za watu binafsi za kufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne ni tatu; nazo ni jitihada, nidhamu na mikakati.

Jitihada katika shule za watu binafsi ziko kwa wanafunzi na walimu wao. Wanafunzi katika shule za watu binafsi wanakariri kwamba wanapata msaada mkubwa kutoka kwa walimu wao madarasani. Kwa upande wa nidhamu ndiyo usiseme.

Shule za watu binafsi ambazo nyingi ni za kidini, zina nidhamu ya hali ya juu. Mkuu wa Shule ya Cannosa iliyotoa mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza, Sista Irene Nakamanya, alinukuliwa akisema kwamba shule yake inafanya vizuri kutokana na wanafunzi kuwa na hofu ya Mungu. Watoto wanalelewa kwa hofu ya Mungu na hawaweki mbele mambo ya dunia hii.

Mikakati mikubwa inayosaidia shule za watu binafsi kufanya vizuri ni miwili; kwanza, ni walimu kujitolea kufundisha kwa bidii na kubobea katika masomo wanayofundisha. Pili, wamiliki wa shule kujali walimu na kuwatimizia mahitaji yao. Walimu wanasikilizwa, wanapewa heshima inayostahili, na wanapatiwa karibu kila kitu wanachokihitaji ikiwa ni pamoja na mikopo ya fedha, magari na nyumba.

Kaulimbiu ya wamiliki wa shule za watu binafsi ni ‘Ukimjali mwalimu mengine yote yatakwenda vizuri’.

Sasa tuangalie sababu zilizotajwa za shule za sekondari kufanya vibaya. Tumeambiwa kuwa sababu moja kubwa ni walimu kukata tamaa. Sababu nyingine ni pamoja na miundombinu mibovu, na mazingira magumu ya kufundishia na ya kujifunzia.

Kwa upande wa walimu kukata tamaa, imeelezwa kwamba walimu wamekata tamaa kutokana na Serikali kutowalipa stahiki zao kama mishahara na motisha. Wakati huo huo kuna walimu wanapandishwa madaraja lakini hawapandishwi mshahara.

Ukweli ni kwamba ari ya walimu kufundisha imeshuka kwa kiwango kikubwa. Kwa hiyo, Serikali isipotoa kipaumbele kwa shule zake ambazo ni kimbilio la Watanzania maskini na wanyonge, hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika siku zijazo.

Lakini hapa tukumbushane kwamba sababu mojawapo ya shule za watu binafsi kufanya vizuri ni nidhamu pamoja na hofu ya Mungu. Ukitaka kusema ukweli shule za Serikali, hasa shule za sekondari za kata, karibu zote hazina nidhamu na wanafunzi wake wanaabudu ngono.

Wanafunzi wa kike na wa kiume hawaheshimiani mitaani na hata kwenye vyombo vya usafiri (daladala). Lugha yao ni chafu wakati wote kiasi cha abiria watu wazima kuwashawishi makondakta wasiwabebe wanafunzi wa sekondari. 

Baadhi yao wanavaa mlegezo (kata kei) na karibu wote wanafunga tai kifuani tofauti na wanafunzi wa shule za msingi na wa shule za watu binafsi.

Kukata tamaa kwa walimu isiwe sababu ya wao kushindwa kufundisha nidhamu na maadili.