China imefanya mazoezi ya kijeshi ya majini kwa siku ya pili kuzunguka Taiwan, huku hali ya wasiwasi ikiendelea kuongezeka baada ya ziara ya Rais Tsai Ing-wen nchini Marekani wiki iliyopita.
Mazoezi hayo ambayo Beijing imeyaita “onyo kali” kwa Taipei – yametumia vikosi vya majini na anga kuiga kuzingira kisiwa hicho.
Taiwan ilisema makumi ya ndege za Kichina ziliruka kwenye kisiwa hicho siku ya Jumapili, wakati meli tisa pia zilionekana.
Operesheni hiyo iliyopewa jina la “Upanga wa Pamoja” na Beijing, itaendelea hadi Jumatatu.
Maafisa wa Taiwan wamekasirishwa na operesheni hiyo, na siku ya Jumamosi maafisa wa ulinzi huko Taipei waliishutumu Beijing kwa kutumia ziara ya Bi Tsai – ambapo alikutana na spika wa Bunge la Merika Kevin McCarthy – kama “kisingizio cha kufanya mazoezi ya kijeshi, ambayo yamedhoofisha sana amani, utulivu na usalama katika eneo hilo”.
Siku ya Jumamosi moja ya meli za China ilirusha duru kutoka kwenye sitaha yake ilipokuwa ikisafiri karibu na kisiwa cha Pingtan, eneo la karibu zaidi la China na Taiwan, shirika la habari la Reuters liliripoti.