Imeelezwa kuwa msukumo uliowekwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu katika Sekta ya Madini umewezesha kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ndogo ya madini ya Viwandani ambapo katika kipindi cha miaka miwili madarakani, mchango wa madini hayo umefikia shilingi Trilioni 1 na bilioni 19 kutoka milioni 451.6.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko wakati akifungua mkutano wa Siku mbili wa Wachimbaji wadogo na wadau wa Madini ya Viwandani ulioandaliwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kushirikiana na Chama Cha Wachimbaji Wadogo Mikoa ya Dar es Salaama na Pwani na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI).

Akizungumza katika ufunguzi, Waziri Biteko amewataka wamiliki wa viwanda kuhakikisha wananunua madini hayo kutokana na bei elekezi iliyowekwa na Serikali huku akiwataka wachimbaji wadogo wa madini hayo kuzalisha madini yenye ubora ili kuepusha hasara kwa wenye viwanda.

Katika hatua nyingine, ameitaka makubaliano yaliyowekwa kati ya STAMICO, taasisi za fedha na wauzaji wa vifaa za uchimbaji madini kutoa matokeo chanya kwa kuwa wajibu wa kuwalea wachimbaji wadogo si hisani bali takwa la kisheria.

Akizungumzia mchango wa wachimbaji wadogo, kwenye maduhuli ya Serikali amesema yamefikia asilimia 40 kutoka asilimia 4 na na kutaka watu wenye ulemavu na wanawake kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta ya madini ili wasibaki nyuma.

Aidha, amepongeza juhudi zilizofanywa na STAMICO kuwafikia wachimbaji mbalimbali na kusema kwamba viwanda vinahitaji maligafi hivyo, mikutano kama hiyo itawezesha ukuzaji wa viwanda nchini kupitia sekta ya madini.