Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Moshi
Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi,imemuachia huru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya.
Sabaya amefutiwa mashtaka saba yaliyokuwa yakimkabili leo Aprili 5,2023 likiwemo la uhujumu uchumi, kuongoza genge la uhalifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Amefikishwa mahakamani hapo ili kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili namba 1/2022.
Upande wa mashtaka umeeleza nia ya kuondoa mashtaka baada ya majadiliano kati ya mshtakiwa na upande wa mashata na kufikia makubaliano ya kisheria.
Makubaliano hayo yamewasilishwa mahakamani hapo kama moja ya vielelezo muhimu vya kesi hiyo, mashtaka mawili mapya yanatarajiwa kufunguliwa dhidi yake.
Msingi wa kesi hiyo, ilidaiwa Sabaya na wenzake wanne walijipatia sh. milioni 30 kutoka kwa mfanyabiashara Alex Swai wakimtishia kutoa taarifa za ukwepaji kodi.
Tangu kufunguliwa kesi hiyo Juni Mosi, 2022 haikuweza kusikilizwa kutokana na sababu mbalimbali za kisheria lakini Septemba 7, 2022 washirika wanne wa Sabaya waliachiwa huru kwa makubaliano ya nje ya Mahakama na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali.
Washirika waliofutiwa kesi ni Sylevester Nyegu, Nathan msuya, John Aweso na Antero Asey ambao mahakama iliwakuta na hatia, kutakiwa kutoa faini sh. 50,000 na fidia y ash. milioni moja kwa muathirika wa tukio hilo ambaye ni Swai.
Mei, 2022 Mahakama Kuu kanda ya Arusha alimuachia huru Sabaya na wenzake wawili waliokata rufaa na kupinga kifungo cha miaka 30 jela katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha.