Takriban watu 26 wamekufa baada ya mfululizo wa vimbunga kuteketeza miji na majiji ya Kusini na Kati mwa Marekani. Nyumba ziliharibiwa na maelfu kuachwa bila umeme baada ya dhoruba kubwa kusababisha uharibifu katika majimbo kadhaa.
Kumekuwa na zaidi ya vimbunga 80 vilivyoripotiwa kwa mujibu wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa.Majimbo yakiwemo Arkansas, Tennessee, Illinois, Indiana, Alabama na Mississippi yote yamekuwa na vifo.
Kimbunga kimoja kilisambaa katika mji wa Arkansas wa Wynne – jamii iliyo umbali wa maili 100 (170km) mashariki mwa mji mkuu wa jimbo hilo, Little Rock.
Vimbunga hivyo hatari vinakuja wiki moja baada ya kimbunga kisicho cha kawaida, cha muda mrefu kusababisha vifo vya watu 26 huko Mississippi.
Kimbunga cha Mississippi wiki iliyopita kilisafiri maili 59 (94km) na kilidumu kwa takriban saa moja na dakika 10 – kipindi kisicho cha kawaida kwa dhoruba kujiendeleza. Iliharibu takriban nyumba 2,000, maafisa walisema. Rais Biden alizuru jimbo hilo siku ya Ijumaa kutoa rambirambi zake.