Katika nchi ambazo najivunia kuzifahamu na kuishi maishani mwangu ni Tanzania. Naipenda nchi yangu kutokana na kila kilichomo ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wake.

Kwa siku ya leo nitakumbushia andiko langu la mwaka mmoja uliopita ambalo niliwahi kumwandikia Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Profesa Dk. Jakaya Kikwete. Nilimwomba aniteue kuwa Kamishna wa Uhamiaji nchini. Hii yote ilikuwa ni kukidhi kiu yangu.

Leo siombi tena nafasi hiyo, bali nimebaini fursa nyingine mzuri ndani ya idara hii, hivyo nimeona heri niombe nafasi hiyo. 

Ukizingatia kuwa Rais wa awamu hii ni mwingine, hivyo litakuwa ni ombi langu la kwanza la kazi kwake, pia pamoja na falsafa yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ ninaahidi kuitumia vyema katika kutimiza lengo langu.

Mimi ni mwanamama raia wa Tanzania, mwenye umri wa mtu mzima, nina akili timamu na vipaumbele katika maisha yangu.

Kutokana na kuona fursa ya kazi katika ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam naomba kupatiwa kazi ya Kamishna wa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam kwa kipindi kifupi cha miezi sita tu.

Naomba kupatiwa kazi hiyo nyeti katika Jiji la Dar ili niweze kuweka mambo yangu sawa. Nimeomba kazi hii kutokana na sifa zake pamoja na fursa adimu zilizomo katika wadhifa huu mkubwa wa mkoa wenye changamoto nyingi.

Kutokana na uzoefu uliopo, nitaweza kujitengenezea mtandao mkubwa na wahamiaji wasiofuata utaratibu kwa kuwawekea kiwango cha fedha za kigeni watakazotakiwa kuwa wananiletea.

Pia kutokana na ugeni wangu mkoani nitajitahidi kuwa karibu na wafanyabiashara wa kigeni watakaokuwa wanakuja kwangu moja kwa moja kuniletea bahasha za kaki ili niwasaidie katika mambo yao.

Kwa kutumia wadhifa huo nyeti mkoani, nitatumia nafasi hiyo kujiandalia maisha yangu ya baadaye na familia yangu kwa kujikusanyia fedha za kigeni pamoja na kuandaa makazi ya maana jijini.

Hii ni moja ya mikakati yangu nitakapokabidhiwa ukubwa huu wa mkoa ambao ni njia mojawapo ya mafanikio. Katu sitaitumia vibaya nafasi hii kama yule mmoja aliyejifanya mchapakazi huku akikataa bahasha na kujijengea maadui waliomuundia kikosi kazi kisha kumuondoa jijini kumpeleka kijijini.

Sitakuwa na hiyana kwa wageni watakaokuwa wakihitaji vibali vya ukaazi nchini. Nitawapatia hata zaidi ya vile wanavyohitaji kupatiwa ilimradi tu waje na kitu kidogo mkononi.

Nitafanya yote haya kutokana na fursa hii adimu kupatikana nchini pia kutokuwapo na ufuatiliaji kwa kiongozi wa aina yangu ambaye ndiye ninayetegemewa mkoani.

Na iwapo afisa yeyote ataamua kuingilia himaya yangu, nitamshughulikia bila hiyana kwa kumtengenezea mtego wa rushwa ili iwe fundisho kwake na maafisa wengine watakaokuwa na viherehere vya kazi na kuniharibia kwa maswahiba wangu.

Katika kipindi ambacho nitakuwa mkubwa wa Uhamiaji Mkoa, nitajitahidi kujipendekeza kwa mabosi wangu huku nikiwasakizia kesi maafisa wangu, nikifanya kila liwezekanalo nisiondolewe katika wadhifa huo.

Ninaahidi ya kuwa katika utendaji wangu wa kazi nitakuwa mchapa kazi mzuri nitakayekuwa na ushirikiano mzuri na vyombo vya habari, hivyo kila jambo nitakalokuwa nalifanya kwa faida ya kuendelea kubakizwa katika nafasi yangu ya muda mfupi, litaonwa na wakubwa wangu hivyo nitaweza kuongezewa muda.

Maelezo yangu ni marefu lakini kutokana na uhaba wa nafasi nalazimika kuishia hapa. Ila chonde chonde nawaomba wakubwa wanipatie nafasi hii ili nitimize kiu yangu japo kwa muda mfupi. Natarajia kupatiwa fursa hiyo niweze kujinufaisha.