Na Tatu Saad JAMHURI MEDIA
Majeruhi pekee wa ajali ya bus la Mwendokasi iliyotokea mnamo Februari 22 mwaka huu jijini Dar es Salaam, Osam Milanzi ameruhusiwa kutoka hospitali baada ya afya yake kuwa timamu.
Milanzi alifikishwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili katika taasisi ya mifupa MOI mnamo Februari 22 mwaka huu ambapo alipatiwa matibabu ya kibingwa katika vitengo vya dharura (EMD), ICU, HDU na wodi 2A.
Meneja uhusiano MOI, Patrick Mvungi amesema Milanzi alipokelewa akiwa na majeraha maeneo ya kichwa, mguu wa kushoto, mkono na bega upande wa kulia.
“Milanzi alipokelewa akiwa ameumia maeneo ya kichwa, mguu wa kushoto, mkono na bega la upande wa kulia” amesema Mvungi.
Hata hivyo Milanzi ataendelea kupewa huduma kama mgonjwa wa nje na atatakiwa kuhudhuria kliniki baada ya wiki mbili.
Aidha Taasisi ya mifupa MOI, imetoa shukrani kwa watanzania wote na vyombo vya habari kwa ushirikiano waliouonesha kwenye kumuombea na kumtangaza Milanzi.