Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu watumie uwepo wa reli ya kimataifa (SGR) kama ni fursa ya kujijenga kiuchumi.
Ametoa wito huo jana jioni wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mwenge, Malampaka mjini, wilayani Maswa.
“Hii reli ujenzi wake ni wa viwango. Reli hii itakuwa na kituo kikubwa sana hapa Malampaka. Kutakuwa na kituo cha kupakia na kushusha abiria lakini pia kutakuwa na kituo kikubwa cha kupakia na kushusha mizigo. Halmashauri pimeni ardhi ili wananchi wapate viwanja vya makazi, wapate hati za kufanyia shughuli za maendeleo,” alisema.
“Wananchi anzeni kujenga nyumba za kulala wageni ili kituo kitakapokamilika na wageni wakianza kushuka wasilazimike kwenda Mwanza moja kwa moja bali walale hapa watuachie hela. Jengeni hoteli za viwango tofauti,” alisisitiza.
Aliwataka viongozi wa wilaya wasiwaache wananchi peke yao bali wawaandalie miundombinu ya ujasiriamali ili akinababa lishe na akinamama lishe wapate maeneo ya kuuzia vyakula vyao kwa ajili ya wageni ambao hawatapenda kula vyakula vya hotelini.
“Wakulima na nyie limeni kwa wingi. Chakula mtakachovuna, mtawauzia watoa huduma kwenye huo mradi. Malampaka ni uchumi na ni mji unaokua kwa kasi,” alisema.
Akijibu hoja ya uhaba wa maji iliyoibuliwa na wananchi hao, Waziri Mkuu alisema Mamlaka ya Maji Vijijini (RUWASA) ilishafanya utafiti na kubaini kuwa maji mengi yaliyoko kwenye eneo hilo hayafai kwa matumizi ya binadamu kwa sababu yana chloride nyingi.
Amesema, kutokana na hali hiyo, Serikali imetenga sh. bilioni 22.4 za mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Tabora ambao utapita maeneo hayo na kuwanufaisha wananchi hao.
Mapema, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa reli ya kimataifa (SGR) kipande cha tano cha kutoka Isaka hadi Mwanza katika vijiji vya Nyashimba na Badi ambako alielezwa kuwa ujenzi wake umefikia asilimia 28.03.
Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli nchini (TRC), Eng. Masanja Kadogosa alisema kipande cha Isaka – Mwanza chenye urefu wa km. 341 kinajengwa kwa ubia wa kampuni ya CCECC na CRCC zote za China na kitagharimu sh. trilioni 3.06.
Akitoa mchanganuo wa wafanyakazi waliopo kwenye kipande hicho, Eng. Kadogosa alisema hadi sasa mradi wa SGR Lot 5 ulikuwa na wafanyakazi 6,771 ambapo 6,210 sawa na asilimia 91.71 ni Watanzania na 561 sawa na asilimia 8.29 ni raia wa kigeni. “Pia kuna sub-contractors 66 na watoa huduma 337 na hivyo kufanya kiasi cha dola za Marekani milioni 35.4 zibakie kutoa huduma za ndani (local content),” amesema.
Naye Mbunge wa Maswa Magharibi, Bw. Mashimba Ndaki aliishukuru Serikali kwa kuweka kituo kikubwa cha kushusha na kupakia abiria hapo Malampaka kwani anaamini kuwa kitahudumia mkoa huo wa Simiyu, mkoa wa Mara na mji wa Kisumu, Kenya.
“Kikijengwa kituo cha kushusha abiria, na cha kushusha na kupakia mizigo hapa Malampaka, tutafaidika kusafirisha pamba kwa urahisi lakini tunaomba pia tujengewe pakilio la ng’ombe kwa sababu sisi ni wafugaji na tuna mifugo mingi,” ameomba.
Kuhusu sekta ya elimu, Bw. Ndaki alisema kwa mwaka huu peke yake, wamepatiwa sh. milioni 660 ambazo zimetumika kujenga madarasa 33. Na katika afya, alisema ndani ya miaka miwili, wamepokea sh. milioni 400 ambazo zimetumika kujenga zahanati nane. “Pia tumejenga vituo vya afya vya Badi, Shishiu na Zibeya kwa gharama ya sh. milioni 300 kila kimoja,” alisema.
Waziri Mkuu amemaliza ziara ya siku tatu katika mkoa wa Simiyu ambako alikagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi kwenye wilaya za Itilima, Bariadi na Maswa.