“Kama ingelikuwa ni baina ya watu wawili binafsi (wanakopeshana fedha), na si kati ya mtu binafsi na benki, basi wasingeliweza kuongeza fedha za kwenye mzunguko wa taifa kwa mkopo, kwa sababu mkopeshaji asingaliweza kukopesha kitu ambacho hana, kama ambavyo mabenki yanavyofanya. Ni mabenki ya biashara na kampuni za dhamana (trust companies) peke yake zinazoweza kukopesha fedha wanazozizuia kutokana na kitendo cha kukopesha.” – Profesa Irving Fisher, Mchumi, kwenye kitabu chake: ‘100% Money’ (1935).

“Suala   ambalo   limekuwapo   kwa   karne   nyingi   na   ambalo   itabidi kupambana nalo mapema au la, ni watu dhidi ya mabenki,” – Lord Acton (1834-1902), Mwanahistoria wa Kiingereza.

Kwenye makala yangu mojawapo mwaka huu, niligusia kuwa asilimia 97 ya fedha zinazokuwapo kwenye mzunguko katika nchi na ulimwengu kwa ujumla, huwa zinazalishwa na mabenki ya biashara.

Kwa ujumla, kuna njia kadhaa ambazo mabenki yanatumia kuzalisha fedha, nazo ni kujikopesha fedha za wateja wao; kutoa mikopo kwa watu binafsi, makampuni na mataifa; ununuzi na uuzaji wa madeni ya taifa (government securities), tozo za bima na ada nyingine za kuendesha baadhi ya akaunti ambazo wateja wao wanafungua.

Katika nukuu ya kwanza hapo juu Profesa Irving Fisher anachokisema, kwa tafsiri, ni kwamba benki za biashara kwa kawaida mbinu ambazo zinatumia kuzalisha fedha mpya ni za kidanganyifu; ni njia ambazo kama tungezitumia mimi na wewe si tu isingaliwezekana bali pia tungalitiwa hatiani kwa kosa la utapeli (fraud); kwani kuuza kitu cha mtu bila idhini yake au ambacho hakipo ni utapeli. Lakini hayo ndiyo ambayo mabenki yanafanya. Fedha za mabenki ya biashara, ingawa bado ni fedha (currency) lakini ni fedha ambazo hazionekani za (kufikirika), ni tarakimu tu za kidijitali; ni fedha ambazo hazigusiki hata  wakati zinahamishwa kutoka sehemu moja  kwenda nyingine au  kutoka nchi  hadi   nchi  kwa   sababu  huwa   ni tarakimu  tu kwenye skrini za makompyuta au maleja (mabuku ya hesabu) na uhamishaji wake kutoka kwenye akaunti moja kwenda kwenye akaunti nyingine huwa unafanyika kwa elektroniki. Kitu ambacho hakibadiliki kati ya fedha za benki kuu (physical currency) na za mabenki ya biashara (digital currency) ni hiki: zote zinazaa madeni ya taifa; zote zinatajirisha mabenki na kufukarisha mataifa na wananchi wake.

Mabenki ndiyo moja ya vyanzo vya umaskini wa watu katika jamii, ndiyo sababu Lord Acton, kwenye nukuu   yangu   ya   pili hapo juu anaongelea ulazima wa   watu kupambana na mabenki ili kujikwamua kutoka kwenye balaa la umaskini na utumwa wa kulipa kodi za mapato zisizo na mwisho na ambazo hazina maslahi yoyote kwa nchi na wananchi.

Moja ya sababu zinazowezesha mabenki ya biashara kuzalisha pesa kwa wingi ni kwa sababu fedha wanazotumia kama mtaji kwenye mchezo wenyewe wa uzalishaji si zao bali za wateja wao – watu binafsi, makampuni na mataifa.

 

Njia ya ukopeshaji

Mchakato unaanza hivi: kila wakati benki ya biashara inatoa mkopo, baada ya mkopaji kusaini mkataba au ahadi ya kulipa hilo deni pamoja na faida (I Owe You –IOU), iwe mkopo huo unatakiwa ulipwe au upevuke baada miezi au miaka, benki inachofanya ni kufungua akaunti ya amana (deposit account) wakati huo huo dhidi ya, au kwa nguvu ya hiyo IOU, yaani ahadi ya mkopaji. Na kwa kufanya hivyo kile kiasi ambacho mtu aliyekopa ameahidi kulipa mara moja kinakuwa au kinageuzwa kuwa ni pesa mpya na ni mali (asset) ya benki, kabla hata huyu mkopaji hajaanza kulipa deni lenyewe.  Benki sasa inaweza kukopesha mtu mwingine hizi  pesa mpya.

Swali la msingi ni hili: kama huyo mteja wao hajaanza kulipa hilo deni, benki inawezaje kuzizalisha hizo fedha au kukopesha fedha ambazo aidha hazijazalishwa au hiyo benki bado haijalipwa? Jibu ni kwamba benki haina hizo fedha; na hicho ndicho  Profesa Fisher anachomaanisha anaposema  wakopeshanaji  binafsi;  yaani wewe na mimi tusingaliweza au tusingaliruhusiwa: “kukopesha kitu ambacho hatuna kama ambavyo mabenki yanafanya.” Yaani mabenki yanaongeza jumla ya fedha katika mzunguko (in circulation), pesa mpya, kwa kuingiza tarakimu tu kwenye leja na hiyo tarakimu yenyewe inaingizwa kutokana na ahadi. 

Mchumi  mmoja,  J.K. Galbraith, aliwahi kusema: “Mchakato unaotumiwa na mabenki kuzalisha pesa ni rahisi kiasi kwamba akili inakataa kukubali”. Alikuwa sahihi.

Aidha, si Profesa Fisher peke yake mwenye kuthibitisha hili; kwa mujibu wa chapisho la David H. Friedman la mwaka 1977 lililotolewa na Idara ya Maelezo kwa Umma ya Federal Reserve Bank ya New York, liitwalo, ‘I Bet You Thought’ linasema: “Mabenki   ya   biashara   yanazalisha   fedha   za   hundi   (cheque   book   money)   kila zinapotoa mkopo kwa kuongeza tu dola mpya za amana (deposit) kwenye mavitabu yao ya mahesabu dhidi ya IOU ya mkopaji”.

Na hiyo IOU hapa huwa ni mkataba mkopaji anasaini wa kuahidi kulipa deni lake la benki pamoja na faida. Kwa muhtasari, mabenki ya biashara yanazalisha au yanazua fedha mpya kwa nguvu za ahadi ya kulipwa na mtu ambaye benki imeamua kumkopesha fedha; na hizo ni fedha ambazo zinakubalika na kuingizwa kwenye mzunguko wa taifa na kwa mwendelezo mzunguko wa ulimwengu. 

Udhaifu wa huu utaratibu upo kwenye hii kweli ya kuwa ni “ahadi ya kulipwa na si ulipwaji wa deni lenyewe” unaotegemezwa kwenye huu uundaji wa fedha mpya. Ikumbukwe kwamba watu wengi wamepata kushindwa kulipa madeni yao, wakati fedha ambazo zilizozalishwa na kusambazwa nchini na duniani kutegemea ahadi zao zinaendelea kuwapo kwenye mzunguko, hali iliyochangia kuleta zahama ya uchumi iliyolipuka, mathalani, mwaka 2008; yenye kuanzia kwenye “sub-prime mortgages”, huko Marekani na ikasambaa dunia nzima kama moto kwenye nyika.

 

Njia ya kujikopesha

Kinyume na imani ya watu wengi, fedha ukishaziweka benki basi kimatendo si zako tena, yaani huwa hutunziwi zile pesa zinapokuwa benki.  Kinadharia ni zako kwa sababu unakuwa na ushahidi wa risiti ya kuziweka kwenye benki husika. Lakini kwa mujibu wa mfumo wa “fractional reserve banking”, ile benki inao uhuru wa kuhifadhi asilimia  kumi tu ya kima ulichoweka na kuchukua   zilizobaki   asilimia   90 na kufanyia chochote inachotaka bila hata kukushauri wewe. Kwa tafsiri inakuwa wateja ndiyo wanazikopesha hizi benki; na pengine ndiyo sababu wanalipa riba (interest) kwa wateja wao hata kama ni kidogo. Hicho kiasi cha hifadhi hutofautiana baina ya nchi; hapa nitatumia mfano wa asilimia kumi.

Kinachotokea ni kuwa mtu, kampuni au taifa wanapoweka kiasi chochote cha fedha benki, tuseme labda Sh 1,000; benki yako inawajibika kuhifadhi Sh 100 (asilimia kumi) kama nilivyosema na kukopesha kwa faida hizo zinazosalia   Sh 900 kwa   mtu   au   taasisi   nyingine   yoyote   ambayo   itakuja kuomba   mkopo   kwenye   benki   hiyo. Na hapo benki huwa mara  moja   imegeuza Sh 1,000 kuwa Sh 1,900 kwa kuingiza   (to credit) shilingi elfu moja kwenye amana (deposits) ya mteja na kukopesha Sh 900 kwa mtu mwingine. 

Waama, mtu anachukua mkopo kwa sababu maalum labda tuseme kununua friji au kitu kingine cha tunu. Mwenye kuuza friji na kuchukua zile mia tisa zilizokopwa naye atakapozipeleka kwenye benki yake kwa “hifadhi” basi hiyo benki yake itawajibika kuhodhi asilimia kumi ambayo  ni  Sh 90 na kukopesha   asilimia   tisini, yaani Sh 810. Hivyo basi huo mchakato  utaendelea kurudiwa tena na tena hadi zile Sh 1,000 zitafikia maelfu, malaki na kuendelea.

Na kwa kawaida, mabenki yanapofanya biashara na makampuni makubwa na mataifa kiasi cha fedha zinazohusika huwa ni kikubwa; tunaongelea mamilioni, mabilioni na matrilioni, siyo elfu.

Na kuhusu tahadhari ya mteja kuja kutaka hela zake ndiyo ile asilimia kumi inayohifadhiwa; lakini hata ikitokea alitaka zaidi ya hiyo asilimia kumi, uzoefu wa benki unaonesha kuwa kwa kawaida ni nadra wateja wote kuja kutaka fedha zao kwa wakati mmoja; na uzoefu huo ndiyo chimbuko la  huu mfumo uitwao ‘fractional reserve system’ yaani kawaida ya kuhifadhi sehemu kidogo ya akiba ya wateja na kukopesha zilizo nyingi. Fauka ya hilo pengo linalosabishwa na utoaji zile asilimia 90, huwa zinafidiwa na IOU ambayo benki inajiandikia (hundi ambayo kiukweli ni  ahadi  tu  isiyo  na  kitu), lakini  pamoja  na  hilo benki inaweza  kutumia ahadi hiyo kununua pesa kutoka benki kuu, kama ni lazima. Pia mabenki ya biashara yanatakiwa kisheria yawe na kiasi cha hifadhi ya fedha kwenye Benki Kuu ya taifa kwa dharura.

 

Mfumo wa ‘fractional reserve’ unatokea wapi?

Miaka mia mbili kabla ya kuzaliwa Kristo (200 BC) sarafu za dhahabu zilianza kutumika; lakini dhahabu ilikuwa si nyepesi kuchukulika, hivyo watu   walipeleka   dhahabu zao kwa wafua dhahabu/masonara (goldsmith) kwa hifadhi kama ambavyo watu leo wanapeleka pesa zao benki wakiamini kuwa wanatunziwa. Yule mfua dhahabu alitoa risiti ya amana aliyokabidhiwa; halafu watu  walianza kutumia  zile risiti  kama noti zinavyotumika leo; risiti hizo   tunaweza kusema ndiyo ‘banknotes’ za awali.

Na hawa wafua dhahabu waligundua kuwa ilitokea mara chache mno watu kuja kutaka dhahabu zao, na hata huyo kumi kwa mmoja walioondokea kuja hawakuja wote wakati mmoja. Hivyo hawa goldsmith wakaanza  biashara ya   kukopesha hii amana ambayo walikuwa wanahifadhi kwa riba. Baada ya muda   si mrefu wafua dhahabu wakaondokea kuwa matajiri wa kuajabiwa. Watawala wakafanya utafiti wa utajiri wa ghafla wa wafua dhahabu.

Matokeo ya utafiti yalipotoka, watawala hawakupiga marufuku huo mtindo bali ulitungiwa sheria na kuidhinishwa. Na hiyo ndiyo sheria ambayo inafuatwa na mabenki yetu leo na imepewa jina maalumu ‘fractional reserve system’, yaani mfumo wa mabenki kuhifadhi kiasi kidogo cha pesa za wateja wao na kukopesha kwa riba zilizo nyingi kwa maslahi ya benki.

 

Njia ya ununuzi na uuzaji wa madeni ya taifa

Njia nyingine kubwa ambayo mabenki ya biashara yanatengeneza fedha ni kupitia ununuaji na uuzaji wa bondi, bili na noti za hazina yaani madeni ya taifa.

Mara kwa mara Hazina zinaitisha mnada wa madeni ya taifa ambako mabenki na makampuni ya ndani na nje ya nchi yanakuja kununua hizo bondi, noti na bili za Hazina. Baada ya muda mabenki hayo yanauzia manunuzi yao ya mnadani Benki Kuu kwa faida.

Mabenki ya biashara na benki kuu karibu zote duniani zinaendeshwa kikupe – kinyonyaji. Kama ulimwengu unataka kuona neema na ustawi wa raia basi utaifishaji wa mabenki na hasa benki kuu za dunia ni muhimu sana, vinginevyo vita duniani hazitakwisha na umasikini utakuwa ni sehemu ya maisha kama ilivyo kuzaliwa na kufa.

Labda nimalizie hii makala kwa wasia ambao Sir Josiah Stamp, aliyekuwa Rais wa Benki ya England miaka ya 1920, na ambaye aliondokea kuwa tajiri wa pili nchini Uingereza zama hizo: “Kama mnataka kubaki watumwa kwa wenye   mabenki (Bankers) halafu mlipe ninyi wenyewe gharama  ya kudumishwa  utumwani, basi muwaache hao (bankers) waendelee kuunda fedha.”

 

Harid Mkali ni  ‘author & journalist’. Anaishi London, Uingereza. Anapatikana kupitia simu: +447979881555, barua   pepe: [email protected] na tovuti: www. haridmkali.com