Na Tatu Saad,JamhuriMedia
Ikiwa ni siku chache zimesalia mabingwa wa ligi ya Tanzania Bara ‘Yanga SC’, kuvaana na TP Mazembe katika mchezo wa kundi D, kombe la shirikisho Barani Afrika, kocha mkuu wa timu hiyo Nassredine Nabi amesema bado wanahitaji kufanya vizuri katika michuano hiyo.
Nabi amesema wana kibarua kigumu katika mshindano hayo, hivyo hataki kuona wachezaji wake wakibweteka ili kuhakikisha wanatimiza malengo waliojiwekea msimu huu kwa kupambana katika kila mchezo.
“Sitaki kuona mchezaji wangu yeyote akibweteka baada ya kufuzu robo fainali kwani bado tuna kibarua kigumu cha kuhakikisha tunafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa pamoja na michezo yetu ya Ligi Kuu,” amesema Nabi.
Nabi amesema wanahitaji kupata ushindi katika mchezo huo wa mwisho dhidi ya TP Mazembe ili kuhakikisha wanamaliza mzunguko wakiwa kileleni katika msimamo wa kundi D wanaloshiriki.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, walianza michuano hiyo kwa kukubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ha Us Monastir, ikawacharaza TP Mazembe mabao 3-1, ikatoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Real Bamako, ikaifunga mabao AS Real Bamako mabao 2-0 kabla ya kuifunga US Monastir mabao 2-0.
Katika msimamo wa kundi D Young Africans ipo kileleni kwa alama 10 sawa na US Monastir wakifuatiwa na AS Real Bamako akiwa na alama 05 na TP Mazembe ikiwa na alama 03, ambapo Young Africans na US Monastir tayari zimeshafuzu hatua ya Robo Fainali.
Young Africans itakuwa ugenini Aprili 02 mwaka huu, katika mchezo wa mwisho dhidi ya TP Mazembe huku ikiwa na Rekodi ya kuifunga mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaa.m.