Na Tatu Saad,JamhuriMedia
Ripoti imeeleza mshambuliaji kutoka nchini Ghana, Benard Morrison ameshapona kwa asilimia 80 na hivyo mchezaji huyo kuweza kuuwahi mchezo wa ligi kuu Tanzani Bara dhidi ya Simba Sc.
Morrison kwa kipindi kirefu amekuwa nje ya kikosi cha Young Africans kwa sababu za kuwa majeruhi, lakini ameshaanza mazoezi binafsi, huku akitarajiwa kujiunga na wachezaji wenzake wakati wowote kuanzia sasa.
Ripoti iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Young Africans, Ally Kamwe imeeleza mambo ni mazuri kwa Morrison na wachezaji kama Denis Nkane ambao walikuwa majeruhi na tayari wameshaanza mazoezi.
“Wachezaji ambao wamebaki kwenye timu kwa kutoitwa kwenye timu zao za taifa wanaendelea vizuri na mazoezi na wale waliokuwa majeruhi wapo sawa.”
“Nkane yeye ameshapona na yupo tayari kucheza michezo ya ushindani na kwa Morrison yeye amepona kwa asilimia 80, nafikiri kwenye michezo ijayo ya ligi anaweza kuwa sehemu ya timu,” amesema Ally Kamwe
Young Africans kwa sasa inajiandaa na mchezo wake wa mwisho wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya TP Mazembe utakaochezwa DR Congo. Baada ya hapo itarudi kujiandaa na mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Geita Gold FC, kisha maandalizi ya Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba SC yataanza rasmi na Morrison anaweza akawepo kwenye mchezo huo.