Na Tatu Saad,JamhuriMedia
Miamba kutoka Azam Complex huwenda ikashindwa kunasa saini ya kocha kutoka DR Congo, Florent Ibenge ambaye amekuwa akitajwa kuwaniwa na klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu 2022/23.
Inaelezwa kuwa mabosi wa klabu ya Al Hilal ya nchini Sudan bado ina mkataba na Ibenge na imeweza kutibua ndoto za Azam kumsajili Ibenge kwa kumuwekea donge nono mezani kocha huyo ili aweze kusalia katika klabu hiyo.
Klabu ya Azam Fc inadaiwa kufanya mazungumzo na kocha huyo ili aweze kutua Jijini Da Es Salaam kwa ajili ya kuchukua mikoba aliyoiacha kocha kutoka Ufaransa Denis Lavagne ya kukinoa kikosi cha timu hiyo.
Hata hivyo matajiri wa Al Hilal nao wamemuahidi kumuongeza maslahi mara mbili ya anachokipata sasa kama atafanikiwa kuifikisha Hilal hatua ya robo fainali LIGI ya Mabingwa ambapo anahitajika kushinda au kutoa sare katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya wababe kutoka Misri, Al Ahly.
Azam FC kwa sasa inatafuta kocha mpya ambaye atapata nafasi ya kukisoma kikosi kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa.